Tanesco yabaini chanzo umeme wa Luku kuisha haraka

Dar es Salaam . Kufuatia malalamiko ya wateja wa umeme wa Luku kuisha haraka katika matumizi, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limefanya ukaguzi wa kitaalamu na kubaini, tatizo hilo linasababishwa na mifumo mibovu ya umeme.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, Tanesco, iliwalazimu kufanya ukaguzi wa kitaalamu katika baadhi ya nyumba ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.

Matokeo ya awali yanaonesha kuwa, katika matukio mengi, tatizo siyo mita za umeme, bali ni mifumo mibovu ya umeme (wiring) majumbani.

Pia, kukosekana kwa elimu sahihi ya matumizi ya umeme na uharibifu wa mifumo ya umeme katika nyumba nyingi, kumetajwa kuwa chanzo cha ongezeko la matumizi ya umeme, ajali za moto na upotevu wa mali na maisha.

Akizungumza leo Januari 27, 2026 baada ya kufanya uchunguzi katika nyumba zilizowasilisha malalamiko, mhandisi wa Tanesco, Ally Mbonde amesema wamefanya uchunguzi katika baadhi ya nyumba na kubaini kuwa, mita nyingi ziko salama na zinapima kwa usahihi.

Hata hivyo, wamebaini kuwa tatizo kubwa ni mifumo mibovu ya umeme iliyofungwa kwenye nyumba hizo.

“Katika nyumba tulizozikagua, tulibaini mteja mmoja alikuwa anatumia takribani uniti 2.5 kwa saa 10, hata akiwa hayupo nyumbani na kuzima vitu vyake vyote. Tuligundua kuna nyaya zisizopaswa kubeba umeme zilikuwa zinabeba umeme,” amesema.

Amesema changamoto kubwa imekuwa mifumo mibovu ya umeme katika nyumba nyingi, hususani nyumba za kurithi au za kupanga, wakazi hawana taarifa kamili kuhusu lini ukarabati wa mifumo hiyo ilifanyika au hali yake ya sasa.

“Watu wengi wanaangalia tu umeme unawaka, taa inawaka, friji inafanya kazi, TV inawaka. Lakini hawatambui kuwa nyaya, soketi na switch navyo vinahitaji kukaguliwa na kuhudumiwa mara kwa mara,” amesema.

Mbonde amesema jamii inapaswa kujijengea utamaduni wa kufuatilia matumizi ya umeme katika maisha ya kila siku, ikiwamo kujua idadi ya uniti zinazotumika angalau kwa siku moja ili kujitathimini kama matumizi yanalingana na mahitaji halisi.

“Ni muhimu mteja akajiridhisha mwenyewe, ajue anatumia uniti ngapi kwa siku. Hapo ndipo anaweza kujua kama matumizi yake yako sahihi, yamebadilika au kuna tatizo,” amesema Mbonde.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanatumia mafundi wa umeme waliosajiliwa (registered contractors) kuwafanyia ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo yao ili kuhakikisha usalama wa nyumba na mali zao.

Amesema mifumo mibovu inaweza kusababisha nyaya za moto na za kurudisha umeme kushikana, hali inayoweza kusababisha moto mkubwa unaoharibu mali au kusababisha vifo.

“Kama wiring ilifanyika miaka 10 iliyopita au zaidi, ni lazima umuite fundi akague viungio vyote kuanzia live wire, neutral hadi earth wire. Haya ni mambo tunayasisitiza sana,” amesema.

Akizungumzia mchango wa hali ya hewa katika matumizi ya umeme, Mbonde amesema matumizi huongezeka zaidi wakati wa joto kali ikilinganishwa na kipindi cha baridi, kutokana na matumizi ya vifaa kama viyoyozi (AC), feni na mifumo ya kupozea majokofu.

“Kipindi cha joto, hasa mikoa ya joto kama Dar es Salaam, matumizi ya umeme huwa juu zaidi. AC zinatumika kwa muda mrefu, friji zinajituma zaidi. Hali ni tofauti na mikoa ya baridi kama Mbeya,” amesema.

Amesema matumizi ya umeme hutofautiana kulingana na mazingira ya kijiografia, hali ya hewa na aina ya vifaa vinavyotumika, hivyo mteja hapaswi kulinganisha matumizi yake moja kwa moja na ya mkoa mwingine.

Pia, amesema kitu kingine kinachochangia matumizi ya vifaa vilivyotumika vinachangiwa na matumizi makubwa ya umeme kwa kuwa, hali ya hewa hutofautiana kutoka nchi moja na nyingine.

George Vicent, mkazi wa Tabata Kisiwani amesema tatizo lililogundulika kwake ni ongezeko la matumizi ya vitu vya umeme ambavyo havikuwepo awali.

“Umeme wa Sh10,000 tulikuwa tunatumia mwezi lakini ghafla tukaanza kutumia siku sita hadi saba lakini leo wamekuja Tanesco kuangalia nimeoneshwa namna ninavyotumia umeme wangu,” amesema Vicent.

Naye, Halman Fred, mkazi wa Tabata Kimanga amesema kwa maelezo aliyoelekezwa na fundi wa Tanesco, kuna haja ya kufanyia kazi licha ya awali kuita fundi kuona tatizo lilipo.

“Nilifuatilia hatua kwa hatua na kuuliza maswali kwanini jambo hilo litokee kipindi cha miezi miwili, majibu yao waliniambia inawezekana, nyaya huwa zinachoka, hivyo zinaweza kusababisha changamoto ya aina hiyo hata kama utakuwa waya mpya,” amesema Fred.

Mwananchi

Related Posts