Serikali ya Tanzania imeiomba Jamhuri ya Watu wa China kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya kisasa ili kujiandaa vyema na uenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, wakati wa hafla ya kusherehekea Mwaka Mpya wa China iliyofanyika katika Ubalozi wa nchi hiyo jijini Dar es Salaam.
Millya amesisitiza kuwa maandalizi ya AFCON 2027 ni zaidi ya michezo, akiyataja mashindano hayo kama fursa ya kimkakati kwa ajili ya mabadiliko ya kiuchumi kwa kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara na utalii, upanuzi wa miundombinu ukihusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja vinavyokidhi viwango vya kimataifa na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania, nchi jirani za Afrika Mashariki na washirika wa kimataifa kama China.
Naibu Waziri amebainisha kuwa uenyeji wa mashindano hayo unahitaji uwekezaji mkubwa katika mifumo ya usafirishaji, huduma za kijamii, na viwanja vya kisasa. China, ikiwa ni mshirika mkuu wa Tanzania katika ujenzi wa miundombinu mikubwa, inatajwa kuwa na mchango muhimu katika kufanikisha azma hiyo ya nchi za Afrika Mashariki.
