
Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, ameagiza mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katika eneo la Ziwa Eyasi, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, akamatwe na kunyang’anywa hati yake ya kusafiria.
Waziri Mkuu, amemwagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Anna Makakala, kumsaka kokote alipo mkandarasi huyo wa Kampuni ya Tunnel, Sadd Ariana.
Dk. Mwigulu, ametoa agizo hilo leo (Machi 6, 2026) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika uwanja wa Mazingira Mjini Karatu.
Awali, Waziri Mkuu, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika Bonde la Eyasi, lililopo km 50 kutoka mjini Karatu.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyowasilishwa, mradi huo unaotekelezwa na serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, utagharimu Sh. bilioni 38.4.
Hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, mwaka huu.
Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha zaidi ya wakulima 2,500 kutoka skimu za Mang’ola Barazani, Maleckchand, Laghangareri, Mbuga Nyekundu, Jobaji na Dumbechand, zenye zaidi ya hekta 5,000.
