
Mwamuzi Ally Mnyupe kutoka Morogoro ambaye alikuwa mwamuzi wa kati wa mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Yanga SC amefungiwa mizunguko mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu akishindwa kuipatia Yanga SC pigo la penati kwa mujibu wa sheria.
Mwamuzi huyo alishindwa kufanya maamuzi sahihi baada ya beki wa Azam FC, Fuentes Mendoza kumchezea rafu mshambuliaji wa Young Africans Sc, Prince Dube ndani ya eneo la penati wakati wa mchezo huo uliomalizika sare tasa katika dimba la Benjamin Mkapa.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ambapo pia klabu ya Yanga imetozwa faini ya Tsh. milioni tano kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wa mchezo huo wakati wakitoka kiwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo huo
Aidha, Azam FC imetozwa faini ya Tsh. milioni tano kwa kosa la kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja huo, ambapo walitumia njia ya kuingilia vyumbani (corridor) kwa shughuli hiyo kabla ya kuanza mchezo, kinyume cha matakwa ya kanuni ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
