
SERIKALI imetoa hakikisho la uhakika wa upatikanaji wa mafuta nchini kwa asilimia 100, huku ikiendelea kuweka mikakati ya kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta ili kuepuka changamoto za upatikanaji katika siku zijazo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema pamoja na malalamiko ya baadhi ya wananchi, hali ya mafuta kwa sasa ni nzuri na inaendelea kufuatiliwa kwa karibu.
Ameeleza kuwa bei ya mafuta hutegemea mambo mbalimbali ikiwemo bei ya soko la dunia, gharama za usafirishaji pamoja na mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni, hususan dola ya Marekani.
“Niitake Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kusikiliza maoni ya wadau wa sekta ya usafiri wakiwemo wamiliki wa vyombo vya usafiri na abiria, ili kuhakikisha huduma zinaboreshwa kwa manufaa ya pande zote,” amesema.
Katika hatua nyingine, Chalamila ametangaza kuwa Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili mkoani Dar es Salaam Aprili 13, 2026 ukitokea Zanzibar, ambapo utakimbizwa kwa siku tano katika wilaya zote kabla ya kukabidhiwa Mkoa wa Pwani Aprili 18, 2026.
1
Amesema Mwenge utakimbizwa katika Wilaya ya Ilala Aprili 13, Kigamboni Aprili 14, Temeke Aprili 15, Ubungo Aprili 16 na Kinondoni Aprili 17, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Chalamila, katika mbio hizo Mwenge utakimbizwa umbali wa kilomita 392.22 ukipitia miradi 35 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 113.57, ambako baadhi ya miradi itazinduliwa, mingine kukaguliwa na mingine kuwekewa mawe ya msingi.
Amesema mbio za Mwenge wa Uhuru zinalenga kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuimarisha umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni, “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”
Aidha, amewataka wananchi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi na shughuli zote za Mwenge ili kutoa heshima kwa tukio hilo muhimu la kitaifa.
Katika hatua nyingine, amegusia suala la wafanyabiashara wa Soko la Mawasiliano lililopata madhara ya moto, akisema serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha wanapatiwa maeneo ya biashara, ambako zaidi ya meza 900 zinatarajiwa kutolewa ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao
