
Kifo cha mwanamitandao maarufu kutoka Miami, Marekani, Ashly Robinson, kimeibua sintofahamu kubwa kimataifa baada ya tukio hilo kutokea akiwa mapumzikoni Zanzibar, Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Zanzibar, tukio hilo lilitokea Aprili 9, 2026, ambapo Robinson alikutwa katika hali mbaya ndani ya chumba cha hoteli aliyofikia. Inadaiwa kuwa alikimbizwa hospitalini akiwa bado hai, lakini alifariki dunia siku iliyofuata, Aprili 10, licha ya juhudi za madaktari kuokoa maisha yake.
Polisi wameeleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha kifo hicho ni kujiua, baada ya madai kwamba alijinyonga ndani ya chumba chake akiwa peke yake. Taarifa hiyo imeeleza kuwa hakuna ushahidi wa kuhusika kwa mtu mwingine katika tukio hilo kwa sasa.
Aidha, imeelezwa kuwa Robinson alikuwa nchini Tanzania kwa ajili ya mapumziko akiwa na mpenzi wake, ambapo kabla ya tukio hilo kulikuwa na taarifa za kutokuelewana kati yao, hali iliyosababisha wawili hao kutenganishwa vyumba na uongozi wa hoteli.
Pamoja na tamko hilo la polisi, bado sintofahamu imeendelea kutawala mitandaoni, huku familia, marafiki na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakieleza kutoridhishwa na maelezo yaliyotolewa, wakitaka uchunguzi wa kina zaidi ufanyike ili kubaini ukweli kamili.
Wakati huo huo, mamlaka zimewataka wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho, huku uchunguzi ukiendelea ili kutoa majibu ya uhakika kuhusu kilichosababisha kifo hicho.
