
Muimbaji wa nyimbo za injili, Martha Mwaipaja, ameonyesha kukerwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni zinazomhusisha na madai ya kuwa katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja na binti yake wa kiroho anayejulikana kwa jina la Joan.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Martha amesema awali alichagua kukaa kimya, lakini kadri siku zinavyosonga amekuwa akipokea mashambulizi makubwa kutoka kwa watu mbalimbali jambo lililomlazimu kuvunja ukimya.
Katika ujumbe wake, Martha amesisitiza kuwa hana uhusiano wowote na madai hayo na amelaani vikali kitendo cha watu kutumia picha zake pamoja na za Joani kusambaza taarifa ambazo anadai si za kweli. Ameeleza kuwa ni wakati sasa wa ukweli kuwekwa wazi na mtu anayehusika na kuanzisha taarifa hizo atajwe hadharani.
Aidha, amezitaka vyombo vya habari vilivyotumia picha zake kuripoti taarifa hizo kujiandaa kutoa maelezo sahihi kuhusu jambo hilo, akisisitiza kuwa anachukulia suala hilo kwa uzito mkubwa.
