
Dar es Salaam. Aliyekuwa Ofisa Habari wa Yanga na sasa Diwani wa Kata ya Kariakoo, Haji Manara ameendelea kuwashangaza wengi baada ya kuibukia kwenye tamthilia maarufu ya Kombolela, jambo lililoibua mjadala miongoni mwa mashabiki wake na wadau wa burudani.
Manara ambaye tayari ameonekana kwenye vipande vya tamthilia hiyo, ameonyesha upande mwingine wa kipaji chake tofauti na ule uliozoeleka wa soka, siasa na utangazaji wa redio.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Manara aliandika maneno yaliyoonekana kuonyesha kufurahishwa kwake na hatua hiyo mpya kwenye sanaa ya uigizaji.
“Another job from fundi Cherehani wako Bwana Chande Jongo,” aliandika Manara.
Kuibukia kwake kwenye Kombolela kumewafanya watu wengi kuamini alikuwa na kipaji hicho tangu zamani. Huku baadhi wakisema huenda amechelewa kuingia rasmi kwenye tasnia ya filamu na tamthilia kutokana na uwezo mkubwa anaouonyesha kwenye mazungumzo na uigizaji wake.
Wadau wengi wa burudani wamekuwa wakieleza Haji ana uwezo mkubwa wa kuzungumza mbele ya watu, kujiamini na kubeba hisia, vitu ambavyo vinaonekana kumpa nafasi nzuri ya kufanya vizuri kwenye ulimwengu wa uigizaji.
Baada ya kuondoka kwenye nafasi yake ya Ofisa Habari wa Yanga, Haji aliendelea kubaki mwanachama wa klabu hiyo huku akiongeza majukumu mengine ikiwemo utangazaji wa redio katika Wasafi Media kabla ya sasa kuingia kwenye tamthilia ya Kombolela.
Kuonekana kwake kwenye tamthilia hiyo kumethibitisha namna Haji Manara alivyo na vipaji vingi, huku mashabiki wake wakisubiri kuona ataishia kwenye uigizaji wa tamthilia pekee au ataingia pia kwenye filamu na miradi mingine ya burudani nchini.
