Mbwa Mwenye Kichaa aua Watoto Wawili Ubungo

Mbwa Mwenye Kichaa aua Watoto Wawili Ubungo
Mbwa Mwenye Kichaa aua Watoto Wawili Ubungo

Mbwa anayedhaniwa kuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa ameibua hofu katika Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam, baada ya kuhusishwa na vifo vya watoto wawili na kujeruhi mtoto mwingine katika matukio yaliyotokea ndani ya kipindi cha wiki mbili.

Watoto waliofariki ni Ibrahim Mkasi (14), mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Mpiji Magoe, na Daniel Sagenge (7), mwanafunzi wa Darasa la Kwanza katika Shule ya Msingi Kibamba.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, watoto hao walipoteza maisha siku kadhaa baada ya kung’atwa na mbwa huyo na kuanza kuonesha dalili zinazohusishwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Mamlaka za serikali za mitaa pamoja na wataalamu wa sekta ya mifugo zimethibitisha kutokea kwa matukio hayo katika maeneo ya Muongoni na Kibwegere, Kata ya Kibamba, pamoja na Mpiji Magoe, Kata ya Mbezi. Zimesema hatua zinaendelea kuchukuliwa kudhibiti mbwa wanaozurura ili kuzuia madhara zaidi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibwegere, Hamphrey Mpili, amesema watoto watatu waliathirika katika matukio hayo, ambapo wawili walifariki dunia na mmoja alipona baada ya kupata matibabu.

“Tumeshatoa taarifa kwa mamlaka husika kwa sababu mbwa hawa wanapaswa kudhibitiwa kabla hawajaleta madhara zaidi,” amesema Mpili.
Mlezi wa Daniel Sagenge, Upendo Massawe, amesema mtoto huyo aling’atwa karibu na nyumbani kwao eneo la Muongoni na kupelekwa Hospitali ya Kimara kwa matibabu. Hata hivyo, hali yake ilibadilika siku chache baadaye na alihamishiwa Hospitali ya Mwananyamala na kisha Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako alifariki dunia.

TAHADHARI KWA WANANCHI

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa mtu yeyote anayeng’atwa na mbwa au mnyama mwingine anayeshukiwa kuwa na kichaa cha mbwa anapaswa:
📌 Kuosha jeraha mara moja kwa maji mengi tiririka na sabuni kwa dakika kadhaa.

📌Kuwahi katika kituo cha afya au hospitali kwa ajili ya tathmini na kupata chanjo ya kuzuia maambukizi (post-exposure prophylaxis) inapohitajika.

📌Kutoa taarifa kwa mamlaka za mifugo au serikali za mitaa ili mnyama husika afuatiliwe.
Kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari unaoweza kuzuilika kwa chanjo na matibabu ya mapema baada ya mtu kung’atwa na mnyama aliyeambukizwa. Kuwahi kupata huduma za afya kunaweza kuokoa maisha.

Chanzo: TSN

Related Posts