
Mwanafalme wa Saudi alikutwa amefariki ndani ya chumba chake cha kifahari cha hoteli jijini London Novemba mwaka jana, huku picha za CCTV zikithibitisha baadaye kwamba alikuwa peke yake katika saa za mwisho kabla ya mwili wake kugunduliwa, uchunguzi wa kisheria umeelezwa.
Prince Abdullah bin Fahad bin Abdullah bin Abdulaziz bin Jalawi Al Saud, mwenye umri wa miaka 29, alikutwa akiwa amelala sakafuni kwenye bafu la chumba chake kilichokuwa ghorofa ya tano katika Hoteli ya Marriott, akiwa bado amevaa nguo zake kikamilifu.
Wafanyakazi wa hoteli walivunja mlango wa chumba hicho kilichokuwa kimefungwa baada ya kugonga mara kadhaa bila kujibiwa.
Maafisa wa usalama pamoja na wahudumu wa dharura walikimbilia eneo la tukio lakini hawakuweza kuokoa maisha yake.
Video za kamera za usalama zilizoonyeshwa wakati wa uchunguzi zilimuonyesha mwanafalme huyo akitoka hotelini peke yake jioni iliyotangulia ili kuvuta sigara, kisha akarudi kwa utulivu katika chumba chake.
Wachunguzi walithibitisha kuwa hakuna mtu mwingine aliyeingia katika chumba hicho katika saa zake za mwisho za maisha.
Matokeo ya vipimo vya sumu mwilini yalionyesha hali ya kutisha kuhusu kile alichokuwa ametumia kabla ya kufariki.
Kiwango cha pombe katika damu yake kilikuwa karibu mara tatu ya kiwango kinachoruhusiwa kisheria nchini Uingereza kwa mtu anayeendesha gari, kiwango ambacho mahakama ilisikia kingeweza pekee kusababisha kupoteza fahamu.
Mbali na pombe, mwanafalme huyo alikuwa pia na viwango vinavyoweza kusababisha kifo vya kemikali nyingine mwilini.
Abdullah alikuwa ameingia katika hoteli hiyo ya Kensington mnamo Novemba 19 akiwa amepanga kukaa kwa wiki moja, lakini hakuwahi kufikisha muda huo.
Uchunguzi pia ulifichua kuwa Prince Abdullah alikuwa akipambana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya kwa muda kabla ya kifo chake.
Gazeti la The Sun liliripoti kuwa mchunguzi wa vifo alihitimisha kuwa hakuna ushahidi wowote unaoonyesha mwanafalme huyo alikusudia kujitoa uhai.
Badala yake, uchunguzi ulihitimisha kuwa alifariki kutokana na mkasa usiokusudiwa.
Mahakama ya Kifalme ya Saudi ilitangaza rasmi kifo cha Prince Abdullah mnamo Desemba 2.
Baadaye, sala ya mazishi ilifanyika katika Msikiti wa Imam Turki bin Abdullah jijini Riyadh, ikihudhuriwa na wanafamilia wa kifalme pamoja na maafisa wakuu wa serikali.
