
Makubaliano ya awali kati ya Simba SC na Wydad AC kuhusu Mwalimu kujiunga na Simba kwa mkopo wa mwaka mmoja yamefutwa.
Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa uongozi wa aliyekuwa Rais wa Wydad, Hicham Ait Menna, lakini yamevunjika baada ya Simba kutokamilisha malipo yaliyokubaliwa, licha ya klabu hiyo kumtangaza mchezaji huyo kupitia kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii.
Hatua hiyo imeleta hasira kubwa kwa uongozi mpya wa Wydad pamoja na Rais mpya wa klabu hiyo. Wydad baadaye ilitoa taarifa rasmi ikimtaka Mwalimu kurejea Casablanca.
Inadaiwa kuwa Wydad walikuwa wakifuatilia kwa karibu kama Mwalimu angecheza mechi yoyote akiwa na Simba katika CECAFA Kagame Cup, huku wakiwa tayari kukusanya ushahidi na kufikisha suala hilo FIFA.
Hata hivyo, Mwalimu tayari amerudi Dar es Salaam akitokea Kigali na kwa sasa anaendelea na mazoezi binafsi akisubiri Wydad kumtumia tiketi ya kurejea Casablanca ili ajiunge na timu kwa maandalizi ya msimu mpya.
Simba sasa italazimika kuanza upya mazungumzo na Wydad ikiwa bado wanahitaji huduma za Mwalimu. Inaelezwa kuwa ada mpya ya mkopo inaweza kuwa kubwa zaidi ya dola 50,000 zilizokubaliwa awali.
