
Uongozi wa Simba SC haraka umebadili uelekeo na kuanza mchakato wa kumsajili mshambuliaji mpya wa hatari, mara baada ya kukosa saini ya Selemani Mwalimu aliyetua kwa watani wao wa jadi, Yanga SC.
Mwalimu, ambaye alikuwa anawaniwa vikali na Wekundu wa Msimbazi, amesajiliwa na Yanga kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja akitokea miamba ya Morocco, Wydad AC, wanaommiliki hadi mwaka 2029.
Bila kupoteza muda, mabosi wa Msimbazi wameanza msako wa haraka wa kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Taarifa za ndani zinafichua kuwa jina la mshambuliaji mzawa, Mgunda, liko kileleni mwa orodha ya wachezaji wanaosakwa.
“Dirisha la usajili bado halijafungwa. Kwenye orodha ya wazawa tunahangaika na Mgunda, lakini mashabiki wakae tayari kwa ‘sapraizi’ kubwa zaidi,” kilisema chanzo cha ndani cha Simba.
Mgunda ana uzoefu wa kutosha ambapo msimu uliopita alicheza AS Vita ya DRC na kufunga mabao mawili, huku msimu wa 2023/24 akipachika mabao sita akiwa na Singida Black Stars. Hata hivyo, Simba itahitaji kufikia makubaliano na Mashujaa FC, klabu inayoshikilia mkataba wake wa mwaka mmoja uliobaki.
Usajili huu unatarajiwa kuongeza chachu na ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Simba huku mashabiki wakisubiri kuona majibu ya viongozi wao dhidi ya usajili wa Yanga.
