
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Crescentius Magori, amewataka mashabiki wa Simba kuwa na utulivu na wasivurugwe na suala la mshambuliaji Selemani Mwalimu ‘Gomes’ kujiunga na Yanga.
Magori ameyasema hayo kabla na baada ya kutua Visiwani Zanzibar ambako kesho Jumatano, Simba itakabiliana na Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia saa 2:30 usiku.
Akizungumza kabla ya kupanda ndege kuelekea Zanzibar leo, Magori amesema kuwa usajili wa ghafla ambao Yanga wameufanya kwa Mwalimu hautakiwi kuwapa presha Wanasimba.
“Mchezaji gani yule? Yaani hilo jambo liitaharuki Simba, Selemani Mwalimu? Yaani huyo mchezaji wa kumlipia bilioni moja kwa mkopo? Simba haiwezi kulipa vitu vya hewa hivyo,” amesema Magori.
Na mara baada ya kutua Zanzibar, Magori amefichua kuwa kiwango cha fedha kilichotumika kumnasa na Yanga kumnasa Mwalimu kwa mkopo, wao Simba hawakuwa tayari kukitoa.
Magori amesema kwamba muda sio mrefu watajibu mapigo kwa kufanya usajili ambao utakuwa gumzo nchini.
“Tunapima tunaona mkopo sio kununua kwa mwaka mmoja tutoe bilioni? Haiwezekani. Pesa ina thamani bwana. Unataka kufurahisha watu siku mbili baada ya hapo unasikia umefungiwa FIFA?
Hamna taharuki. Angekuwa hata mchezaji wa kikosi cha kwanza. Hatufanyi mambo hayo sisi. Tutapata mchezaji pengine mzuri kuliko huyo. Wewe tulia tutatangaza. Nyie tulieni, hii ni Simba. Simba ni imara tena imara kweli kweli,” amesema Magori.
Wachomoa mmoja Mashujaa
Baada ya Yanga kumnasa Mwalimu ambaye Jumamosi alitambulishwa na Simba kama mchezaji wao mpya, Simba harakaharaka imeingia sokoni na kumnasa mshambuliaji mmoja mzawa.
Mchezaji huyo ambaye Simba inasubiria kumtangaza tu hivi sasa ni Ismail Mgunda kutoka Mashujaa FC.
Inaripotiwa kwamba Mashujaa FC na Simba zimefikia makubaliano ya kuuziana mchezaji huyo aliyewahi kuitumikia pia Tanzania Prisons.
Wakati Mashujaa FC ikielekea Tanga, Mgunda amelazimika kubadili uelekeo na kuja Dar es Salaam ili asafirishwe haraka kuelekea Zanzibar.
Uhamisho wa kushtua
Licha ya kumnasa Mgunda, Simba imeahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha ndani ya muda wa saa 48 inasajili mchezaji mwenye jina kubwa kama njia ya kujibu mapigo kwa Yanga iliyomchukua Mwalimu mikononi mwao.
“Usajili haujaisha na hili lililotokea kwa Mwalimu lazima tulipe kisasi. Tutahakikisha maumivu ambayo baadhi ya Wanasimba wanayapata kwa Mwalimu kuondoka, ndio wapinzani watayapata kwa mchezaji tutakayemtambulisha ndani ya hizi siku mbili,” amesema mmoja wa vigogo wa Simba ambaye hakupenda jina lake kutajwa.
Kumekuwa na tetesi kuwa Simba inamuwinda nyota wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye pia anawaniwa na Yanga.
