
DILI LAIVA MOROCCO: AS FAR Rabat Yaongeza Dau la Allan Okello, Yanga Yamweka Sokoni Baada ya Aziz Ki Kurejea
DAR ES SALAAM – Upepo wa usajili ndani ya klabu ya Yanga SC umeendelea kuchanganya baada ya mabingwa hao wa Tanzania kufikia maamuzi ya kumuweka sokoni kiungo wao mshambuliaji raia wa Uganda, Allan Okello. Hatua hii imekuja mara baada ya miamba hiyo kukamilisha mchakato wa kumrejesha kikosini mchezaji wao nyota, Stephane Aziz Ki.
Kurejea kwa Aziz Ki kumerahisisha maamuzi ya Uongozi wa Yanga kumpisha Okello ili kusawazisha idadi ya wachezaji wa kigeni pamoja na uwiano wa kikosi katika eneo la usambazaji.
Hali hiyo imewapa mwanya miamba ya soka nchini Morocco, AS FAR Rabat, kuongeza dau lao ili kupata saini ya Mwaganda huyo kabla ya dirisha la usajili kufungwa, kufuatia ushindani mkali wa awali kutoka kwa Wydad Casablanca. Mazungumzo kati ya viongozi wa Yanga na wakala wa AS FAR Rabat yapo hatua za mwisho kukamilisha uhamisho huo.
