
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), nchini Kenya, Douglas Kanja, ameamuru maofisa wanaokuwa kazini wakati mtuhumiwa anafariki akiwa kizuizini kusimamishwa kazi mara moja, wakisubiri uchunguzi wa mazingira ya kifo hicho.
Kanja amesema agizo hilo linawahusu ofisa anayesimamia Kitabu cha Matukio ya Polisi (O.B), askari anayelinda seli na ofisa wa zamu.
Akizungumza na makamanda wa polisi wa mikoa, Kanja amesema maafisa hao wanapaswa kuwajibishwa katika kila kisa cha kifo kinachotokea ndani ya seli za polisi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini kilichotokea.
“Kifo chochote kinachotokea katika seli za polisi, ofisa anayerekodi O.B., askari anayelinda seli na ofisa wa zamu lazima wasimamishwe kazi mara moja, huku uchunguzi ukiendelea. Hilo ni jambo ambalo nyinyi kama makamanda lazima mhakikishe linafanyika,” amesema Kanja.
Kanja pia amewakosoa makamanda wa polisi kwa kushindwa kudhibiti utovu wa nidhamu miongoni mwa maofisa walio chini yao, akisema watakaoshindwa kuchukua hatua watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Naye Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi anayesimamia Huduma ya Polisi ya Utawala, Gilbert Masengeli, amesema makamanda watawajibishwa iwapo uhalifu utaongezeka katika maeneo yao ya kiutawala.
“Uhalifu ukiongezeka katika maeneo yenu ya uwajibikaji, nyinyi kama makamanda mtakuwa wa kwanza kuulizwa maswali. Hili ni onyo dhidi ya uzembe katika uongozi,” amesema Masengeli.
Kanja pia ameonya kuwa makamanda watakaoshindwa kudhibiti magenge ya uhalifu katika maeneo yao watakabiliwa na hatua za kinidhamu, ikiwemo kushushwa cheo.
Onyo hilo linakuja huku kuongezeka kwa shughuli za magenge ya uhalifu kukizua wasiwasi kuhusu usalama nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
BBC
