
Watu Wanne Wafariki Kwenye Ajali ya Basi la Abood na IST Bunju
Watu wanne wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha basi la Abood na gari dogo aina ya Toyota IST katika eneo la Bunju Sokoni, Barabara ya Bagamoyo, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo, Septemba 8, 2026, ajali hiyo ilitokea Septemba 7 majira ya saa 7:40 usiku. Basi hilo (Yutong, T 235 EMJ) lililokuwa likiendeshwa na Christivian Steven Shemuhilu (38) kuelekea Tanga, liligongana uso kwa uso na Toyota IST (T 274 ERU) iliyokuwa ikiendeshwa na Hamad Mohamed Juma (37).
Chanzo cha ajali kimetajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa basi kufuatia kuhama njia yake na kujaribu kupita gari jingine (overtake) bila kuchukua tahadhari.
Orodha ya waliopoteza maisha:
-
Hamad Mohamed Juma (37), Dereva wa IST, mkazi wa Mtoni Mtongani.
-
Edward Kimanyara, Mstaafu, mkazi wa Yombo Dovya.
-
Magdalena Manyenga (45), mkazi wa Temeke.
-
Melina Emmanuel Kayoka (42), mkazi wa Yombo Kisiwani.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa ajili ya taratibu za utambuzi na hifadhi.
