
Aliyekuwa mume wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Hafidh Ameir Hassan amezikwa leo Jumatatu, Septemba 7, 2026, katika kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, akiacha wajane wawili, watoto wanne na wajukuu 15.
Wasifu wa marehemu umesomwa na Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Shabaan Kisu, wakati wa maziko hayo, umeeleza kuwa Hafidh alizaliwa Januari Mosi, 1946, katika kijiji cha Kisakasaka, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Maziko hayo yameongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na vyama vya siasa.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Safari ya elimu
Kwa mujibu wa Kisu, Hafidh alianza elimu ya msingi katika Shule ya Kombeni Shakani, Wilaya ya Magharibi B na kuhitimu mwaka 1960.
Baadaye aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Tumekuja, Mkunazini na kuhitimu mwaka 1965.
“Katika maisha yake, marehemu aliendelea kutumia fursa mbalimbali za elimu na mafunzo kujiendeleza kitaaluma, hususani katika fani za ualimu na kilimo,” amesema Kisu.
Amesema 1970, Hafidh alijiunga na Chuo cha Ualimu Zanzibar na kuhitimu 1973 kabla ya kuajiriwa kama mwalimu na kufundisha katika shule mbalimbali Tanzania.
Mwaka 1980 alichaguliwa kwenda kusomea masuala ya kilimo katika Chuo cha Kilimo Uyole, Mbeya, hatua iliyomwezesha kuongeza maarifa na ujuzi katika taaluma hiyo iliyokuwa sehemu muhimu ya maisha yake ya kazi.
Mwaka 1982 aliajiriwa kuwa mkufunzi wa masomo ya kilimo katika Shule ya Fidel Castro, Pemba.
Miaka minne baadaye, mwaka 1986 alipata fursa ya kwenda Sri Lanka kujiendeleza katika taaluma ya kilimo kwa ngazi ya stashahada na alihitimu mwaka 1988 akiwa amebobea katika kilimo cha minazi.
Aliporejea Zanzibar mwaka huo, aliendelea na kazi katika Wizara ya Kilimo.
Masomo Uingereza
Kisu amesema Hafidh aliendelea kutafuta fursa za kuongeza ujuzi wake kitaaluma na mwaka 1990 alikwenda Uingereza kusoma shahada ya uzamili katika fani ya ufundi wa mitambo ya kilimo.
“Baada ya kuhitimu, alirejea Zanzibar na kuendelea na kazi katika Wizara ya Kilimo hadi alipostaafu mwaka 2005,” amesema Kissu.
Baada ya kustaafu utumishi wa Serikali, Hafidh aliendelea kufundisha katika Chuo cha Kilimo Kizimbani, Unguja.
Kabla ya kifo chake, Septemba 7, 2026, Kissu amesema alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo na alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali.
Viongozi walivyoshiriki
Maziko hayo yamehudhuriwa pia na viongozi wastaafu na waliopo madarakani, akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah.
Wengine ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete; Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume; Rais mstaafu wa Zanzibar wa awamu ya saba, Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Othman Masoud Othman.
Kwa upande wa CCM, waliohudhuria ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdi Mahmoud Abdi.
Maziko hayo pia yamehudhuriwa na mawaziri na manaibu mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali, dini na vyama vya siasa.
Hafidh ameacha historia ya utumishi wa umma iliyojikita zaidi katika elimu na kilimo, taaluma alizozitumikia kwa miaka kadhaa kabla na baada ya kustaafu.
