
Kurejea Kwa Clement Mzize Tatizo Jipya Ligi Kuu Bara
Clement Mzize leo amerejea kwenye kikosi cha Yanga kwa mara ya kwanza tangu alipoumia, baada ya kukaa msimu mzima uliopita bila kucheza mchezo wowote wa ligi.
Kwa mtazamo wangu, Mzize bado ni yule yule. Ubora wake haujapotea. Ni ule ubora uliowafanya Wydad Casablanca kumhitaji kwa dau lililoripotiwa kuwa zaidi ya Sh bilioni 5, lakini Yanga wakasema bado wana matumizi naye na hawakuwa tayari kumuacha.
Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba Mzize bado anahitaji muda kurejea kwenye kiwango chake cha juu. Anaonekana kucheza kwa tahadhari, jambo linaloweza kusababishwa na hofu ya kuumia tena. Pia, baada ya kukaa muda mrefu nje, ni kawaida kuwa na changamoto ya kujiamini kwenye mechi pamoja na utimamu wa mwili kutokuwa kwenye kiwango chake cha juu.
Haya yote ni sehemu ya mchakato wa mchezaji anayerejea baada ya jeraha.
Lakini jambo kubwa ni kwamba Mzize amerudi. Na kurejea kwake kunaongeza kitu muhimu sana kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga—kasi, nguvu, uwezo wa kushambulia nafasi na ubora wa kumalizia mashambulizi.
Akiendelea kupata dakika na kurejesha utimamu wake wa mwili pamoja na kujiamini, Mzize anaweza kuwa silaha muhimu sana kwa Yanga.
Wapinzani wa Yanga, jipangeni. Mzize amerudi
