
‘Marufuku kuuza dawa za meno kwenye usafiri wa umma’
WIZARA ya Afya, Idara ya Kinywa na Meno, imepiga marufuku na kuwaonya wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma, kuruhusu matangazo ya matibabu na dawa za kinywa na meno, ndani ya usafiri, huku watangazaji hao, wakipotosha na hawana ujuzi wowote unaotambuliwa kisheria.
Imesema kuendelea kuwaruhusu wapotoshaji hao ni kuvunja sheria za nchi, hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, wakiwamo wamiliki wa chombo husika, dereva na kondakta wa chombo husika pamoja na mpotoshaji mwenyewe.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Kinywa na Meno, Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo, alisema hayo jana, akizungumza na gazeti hili, kuhusu afya ya kinywa na meno kwa umma.
Dk. Nzobo, ambaye ni bingwa bobezi katika afya ya kinywa na meno, alisema vyombo vya usafiri, vizingatie kutoruhusu watu kutoa elimu za afya ya kinywa na meno kwenye vyombo vyao vya usafiri.
“Wizara inapenda kutoa angalizo kwa watu wote ambao siyo wanataaluma ya kinywa na meno, ambao pia hawana usajili wala leseni kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika, kuacha mara moja kutoa elimu na matangazo ya upotoshaji katika afya kinywa na meno za watanzania na masuala mengine ya afya.
“Kama mtu anatamani sana kujihusisha na masuala ya kutoa elimu ya kinywa na meno kwa jamii, Wizara inamshauri mtu huyo aende kusoma elimu ya kinywa na meno kwenye vyuo vinavyotambuliwa na serikali kuanzia ngazi ya stashahada ya utabibu wa kinywa na meno au shahada ya udaktari wa kinywa na meno.
“Meno yakitoboka, kuoza hutibiwa hospitali na daktari wa kinywa na meno kwa kutumia dawa zilizopo hospitali baada ya kukufanyia uchunguzi wa kina,” alisema Dk. Nzobo.
Alisema kwamba watu ambao hawana taaluma ya kinywa na meno na wala hawajasajiliwa na kupewa leseni na Baraza la Madaktari Tanganyika (MEDICAL COUNCIL OF TANGANYIKA), wamekuwa wakiwadanganya watanzania kupitia mitandao ya kijamii na kwenye mabasi ya masafa marefu.
“Wanauza dawa za kupigia mswaki meno ambazo zinatibu meno yaliyotoboka, watu hawa wamekuwa wakisababisha matatizo makubwa sana kwenye eneo la kinywa na meno, kwani wananchi wamekuwa wakiishia kuja hospitali wakiwa wamepata jipu la jino.
“Jipu la jino hutokanana na jino lililooza kwa muda mrefu, ambalo halijapatiwa matibabu yanayotakiwa kuondoa sehemu ya jino iliyooza na kuliziba kwa dawa za hospitali au kulifanyia matibabu ya mzizi wa jino (root canal treatment).
Alieleza kuwa baadhi ya dawa za meno zina viambata vinavyofanya jino linalouma kupigwa ganzi na kulinyamazisha kuuma huku likiendelea kuoza na kutengeneza usaha kimya kimya ndani ya jino na taya kwa muda mrefu na baadae mtumiaji kuja kushtuka shavu limemvimba na kuanza kupata maumivu.
“Jipu la jino linajitengeneza bila ya yeye kutambua. Gharama za kutibu jibu la jino ni kubwa na madhara ya jipu la jino ni kuozesha mfupa wa taya (Osteomylitis).”
