
Mwandishi wa habari mashuhuri wa michezo kutoka Uhispania, Edu Aguirre ambaye anajulikana kuwa rafiki wa karibu sana wa Cristiano Ronaldo amefichua machache kuhusu sakata la Ronaldo kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa ya Ureno akibainisha kuwa nyota huyo aliondoka kambini baada ya kujisihi kusalitiwa na kocha Jorge Jesus kutokana na ahadi ya uongo aliyopewa.
Kwa mujibu wa mwandishi huko, kwenye mechi dhidi ya Norway, kocha Jesus alimwambia Ronaldo apashe (warm-up) kwa dakika 30 lakini mwishowe akamwacha benchi na hakumuingiza uwanjani, jambo lililomkasirisha nahodha huyo wa Ureno.
Aidha baada ya mchezo huo, kulifanyika kikao cha faragha kilichomhusisha Cristiano Ronaldo, kocha Jorge Jesus, na Rais wa Shirikisho la Soka la Ureno (FPF), Pedro Proença ambapo katika kikao hicho, Jorge Jesus alimuomba radhi Ronaldo faragha kwa kitendo cha kumkalisha benchi na kumfanyisha mazoezi bila kumtumia.
Kocha huyo aliahidi mbele ya Ronaldo kuwa angeurudia msamaha huo hadharani kwenye mkutano na waandishi wa habari na kukiri kuwa alifanya makosa lakini hakufanya hivyo badala yake akizungumza tofauti kabisa kwenye mkutano na Waandishi wa habari hatua iliyomghadhibisha Ronaldo.
Baada ya kocha huyo kufika mbele ya waandishi wa habari alibadilisha lugha kabisa na kudogosha tukio hilo akisema hakuna mzozo wowote, na akatamka kuwa “Cristiano ni mchezaji kama wengine, mimi ndiye ninayeamua”, hatua iliyomfanya Ronaldo kuamua kufungasha virago na kuondoka kambini kwenda Madrid, akiona hakuna tena misingi ya kuaminiana.
Mwandishi huko amedai nyota huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid hakukasirishwa na kukaa benchi, bali alilipuka kwa hasira na kuhisi kudhalilishwa na kusalitiwa kwa sababu kocha wake alimwambia maneno mengine faragha na kwenda kusema uongo hadharani ili kuonyesha kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka.
