
TMA: Mvua Kutarajiwa Kunyesha Mfululizo Mikoa Hii Saa24 Zijazo Kuanzia Saa3 Usiku
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo, Jumatano, Oktoba 7, 2026, ikieleza kuwa maeneo mbalimbali nchini yanatarajiwa kushuhudia hali tofauti za hewa, zikiwemo mvua, ngurumo za radi na vipindi vya jua.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkoa wa Kigoma unatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache pamoja na vipindi vya jua. Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Kagera, Geita, Mwanza na Mara nayo inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua.
TMA imeeleza kuwa Visiwa vya Unguja na Pemba vinatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua nyepesi katika maeneo machache pamoja na vipindi vya jua. Mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, pamoja na maeneo ya Pwani, ikiwemo Visiwa vya Mafia, nayo inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi na vipindi vya jua katika baadhi ya maeneo.
Katika maeneo ya kaskazini, mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara inatarajiwa kupata vipindi vya jua huku hali ya hewa ikibadilika katika baadhi ya maeneo. Mikoa ya Morogoro, Lindi na Mtwara pamoja na Tabora na Katavi pia imepewa tahadhari ya uwezekano wa mvua katika baadhi ya maeneo kulingana na mwenendo wa hali ya hewa.
Kwa upande wa nyuzi joto, baadhi ya miji nchini zinatarajiwa kufikia viwango vya juu vya joto vya kati ya nyuzi 27 hadi 33°C, huku viwango vya chini vikitarajiwa kushuka hadi kati ya nyuzi 11 na 23°C katika maeneo mbalimbali. TMA pia imesema upepo wa pwani unatarajiwa kuvuma kwa kasi ya hadi kilomita 30 kwa saa, kutoka kusini mashariki kwa Pwani ya Kaskazini na kutoka mashariki kwa Pwani ya Kusini.
Aidha, TMA imesema hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi, hivyo wananchi wanaotumia shughuli za baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari. Kwa matarajio ya Ijumaa, Oktoba 9, 2026, TMA imesema vipindi vya mvua vitaendelea katika maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria. Wananchi wanashauriwa kufuatilia taarifa rasmi za TMA na kuchukua tahadhari kulingana na hali ya hewa katika maeneo yao
