Muonekano wa Vitambulisho Vipya vya NIDA

Muonekano wa Vitambulisho Vipya vya NIDA
Muonekano wa Vitambulisho Vipya vya NIDA

Muonekano wa Vitambulisho Vipya vya NIDA

Huu ndio mwonekano mpya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezindua kitambulisho kipya cha Taifa cha kisasa chenye teknolojia ya leza inayolenga kuongeza uimara, kuimarisha usalama na kupunguza uwezekano wa kughushi taarifa za utambulisho wa mwananchi.

Uzinduzi huo umefanyika jana Novemba 18, 2026, ukiwa sehemu ya maboresho ya mfumo wa vitambulisho vya Taifa yanayolenga kuongeza matumizi yake katika huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kidijitali. Kitambulisho hicho kipya kimeongezewa uwezo wa kuhifadhi programu za kidijitali kutoka nne zilizokuwepo awali hadi nane.

Mabadiliko hayo yanatarajiwa kupanua matumizi ya kitambulisho katika mifumo mbalimbali ya huduma, kadiri taasisi na mifumo yake itakavyounganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Hatua hiyo inalenga kuwezesha kitambulisho kutumika zaidi ya kazi ya kuthibitisha utambulisho wa mtu katika mazingira ya kawaida.

Akizungumza kuhusu maboresho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ununuzi wa kadi mpya pamoja na mashine tano za kisasa zitakazotumika katika uzalishaji wa vitambulisho.

Amesema mashine hizo zina uwezo wa kuzalisha vitambulisho 2,800 kwa saa, hatua inayolenga kuongeza kasi ya uzalishaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wanaohitaji vitambulisho vya Taifa.

Tofauti kubwa kati ya kitambulisho kipya na mfumo uliokuwa ukitumika awali ipo katika teknolojia ya uchapishaji wa taarifa. Katika mfumo wa zamani, taarifa za mwananchi zilikuwa zikichapishwa kwa kutumia wino, lakini teknolojia mpya inatumia mionzi ya leza kuchora picha na taarifa ndani ya tabaka za kadi.

Teknolojia hiyo inaongeza kiwango cha usalama kwa kufanya taarifa zilizowekwa kwenye kitambulisho kuwa ngumu kubadilishwa au kughushi. Aidha, matumizi ya mfumo huo yanaongeza uimara wa kadi kwa kuwa taarifa zinaingizwa ndani ya tabaka zake badala ya kutegemea uchapishaji wa kawaida juu ya uso wa kadi.

Katika uzinduzi huo pia kumezinduliwa programu ya NIDA Wallet, inayomwezesha mwananchi kuhifadhi utambulisho wake wa kidijitali ndani ya simu ya mkononi. Kupitia programu hiyo, mwananchi ataweza kuthibitisha taarifa zake anapohitaji kupata huduma zinazotolewa na taasisi ambazo mifumo yake itaunganishwa na NIDA.

NIDA Wallet inalenga kurahisisha upatikanaji na matumizi ya taarifa za utambulisho bila mwananchi kutegemea kitambulisho cha kawaida pekee kila anapohitaji kuthibitisha taarifa zake.

Kwa maboresho hayo, Serikali imeongeza uwekezaji katika miundombinu ya utambuzi wa wananchi, huku teknolojia mpya, mashine za uzalishaji na programu ya kidijitali vikitarajiwa kupanua uwezo wa mfumo wa vitambulisho vya Taifa nchini Tanzania.

Related Posts