
Waziri Kwagilwa Afunguka: Acheni UTANI wa El Nino
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa
amewataka Watanzania kuacha kubeza tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa hali ya hewa kuhusu mvua kubwa za El Niño, akisema baadhi ya Wananchi wamefikia hatua ya kuidai Serikali mvua hizo badala ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mkoani Iringa, Kwagilwa amesema Serikali imekuwa ikitoa elimu na tahadhari katika mikoa 14, lakini baadhi ya Wananchi wamekuwa wakizichukulia taarifa hizo kama ahadi ya mvua zinazopaswa kunyesha.
“Makamu wa Rais, baada ya kuwa tumezunguka mikoa yote 14 kutoa tahadhari hii, sasa hivi tukipita Watanzania wanatudai mvua ya El Niño,” amesema Kwagilwa.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kufanya usafi wa mazingira, kuzibua mitaro na kuhakikisha njia za kupitisha maji hazizibwi na taka, ili kupunguza hatari ya mafuriko na madhara mengine yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.
