
Aliyedai Ametekwa na Wasiojulikana Akamatwa Arusha
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limemkamata Vivian Jackson Salekwa, Mkazi wa Majengo Jijini Arusha kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa na Watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo taarifa za kutekwa kwa Mwanamke huyo ziliripotiwa Oktoba 10, 2026, zikieleza kuwa alichukuliwa na Watu wasiojulikana waliokuwa wakitumia gari jeusi katika eneo la Majengo na kupelekwa kusikojulikana.
Kamanda Masejo amesema baada ya uchunguzi uliofanyika, Oktoba 16, 2026, Polisi walibaini kuwa Vivian hakuwa ametekwa, bali anadaiwa kupanga tukio hilo ili kuficha kesi ya kutishia kuua inayomkabili mpenzi wake, Castus Bagambisa ambayo inaendelea kuchunguzwa Mkoani Kilimanjaro.
Aidha, uchunguzi wa Polisi umeeleza kuwa Vivian alimtuma mfanyakazi wake wa nyumbani, Mariam Mwinjuma kuwafikishia Wazazi wake taarifa kuwa ametekwa, wakati yeye akiwa amekwenda kujificha.
Jeshi la Polisi limesema linawashikilia Watu watatu, ambao ni Vivian Jackson Salekwa, Mariam Mwinjuma na Castus Bagambisa, kuhusiana na tukio hilo kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.
