EDO KUMWEMBE: Yanga Inapaswa Kurudi Congo na Ivory Coast Kwenye Usajili

EDO KUMWEMBE: Yanga Inapaswa Kurudi Congo na Ivory Coast Kwenye Usajili
EDO KUMWEMBE: Yanga Inapaswa Kurudi Congo na Ivory Coast Kwenye Usajili

EDO KUMWEMBE: Yanga Inapaswa Kurudi Congo na Ivory Coast Kwenye Usajili

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Edo Kumwembe, ametoa ushauri mzito kwa viongozi wa klabu ya Young Africans (Yanga SC) kuhusu mtindo wao wa usajili na aina ya wachezaji wanaopaswa kuwasajili kuelekea madirisha yajayo ya usajili.

Nje ya changamoto za kufuata au kuacha mapendekezo ya makocha, Kumwembe anasisitiza kuwa viongozi wanatakiwa kufikiria kwa upana zaidi kuhusu mataifa wanayoyapa kipaumbele wakati wa kusaka wachezaji wa kigeni.

1. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC): Chimbuko la Roho ya Kupambana

Edo Kumwembe anaeleza kuwa historia inaonyesha Yanga imekuwa na bahati kubwa na wachezaji kutoka nchini Congo kuliko taifa jingine lolote.

“Wachezaji kutoka Congo wana juhudi na wanajua maana ya kazi. Hata kama mchezaji hana kipaji kikubwa sana, kile kidogo alichobarikiwa anakitumia kwa 100% kwa manufaa ya timu. Ukipata wachezaji watano wazuri kutoka Congo, unaweza kujenga timu bora zaidi,” anafafanua Kumwembe.

Akimulika mafanikio ya hivi karibuni, anakumbusha kikosi kilichofika Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF CC) kikiwa na wimbi la wachezaji kutoka Congo kama Fiston Mayele, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Yannick Bangala, Tuisila Kisinda, na Jesus Moloko.

Kikosi hicho kilikuwa tishio kiasi cha kuwafanya wachambuzi na mashabiki kuhoji kwa utani kama hiyo ilikuwa ni timu ya mpira au bendi ya muziki kutoka Congo.

2. Ivory Coast: Nyumbani wa Mafundi wa Mpira

Nje ya Congo, Edo Kumwembe anaishauri Yanga kuelekeza macho yao nchini Ivory Coast, sehemu ambayo imeleta majina makubwa na mafundi wa mpira klabuni hapo kama Pacôme Zouzoua, Yao Kouassi (Yao Yao), na Kipré Jr.

Anasisitiza kuwa unapoenda Ivory Coast, lengo liwe ni kuchukua wachezaji wa kiwango cha juu (Top Players) na sio wachezaji wa kiwango cha kawaida.

“Unapokwenda kununua wachezaji huko, mjitahidi hata kubomoa timu moja wapo yenye ushindani. Muunganiko wa mafundi wa Ivory Coast ukichanganywa na juhudi za Wacongo, unapata timu hatari sana barani Afrika.”

Kila Klabu na Bahati Yake: Mchanganuo wa Mataifa

Kumwembe anafafanua kuwa ingawa usajili una kipengele cha bahati, klabu kubwa za Tanzania zina mataifa ambazo zimekuwa zikipata nazo mafanikio zaidi:

  • Yanga SC: Congo & Ivory Coast

  • Simba SC: Zambia

  • Azam FC: Zimbabwe

“Yanga inabidi irudi kwenye hizo nchi haraka sana iwezekanavyo. Hata kama watasajili wachezaji kutoka mataifa mengine, isitokee kuwa wengi kuliko kutoka kwenye haya mataifa mawili makuu,” aliongeza.

Tathmini ya Kikosi cha Sasa

Akitolea mfano mchezo wa Siku ya Mwananchi, Edo Kumwembe ametanabaisha kuwa timu iliyocheza na Yanga siku hiyo ilikuwa na wachezaji wengi bora kuliko kikosi cha sasa cha Yanga, jambo linalothibitisha kuwa viongozi wamesahau kidogo misingi iliyoijenga timu hiyo kuwa imara miaka ya hivi karibuni.

Related Posts