
Kaka wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye ni Wakili Allute Lissu Mughwai, amefariki dunia saa 8 usiku wa kuamkia leo, Novemba 1, 2026, wakati akipatiwa matibabu hospitalini Jijini Arusha.
Akizungumza na AyoTV, Dada wa Marehemu, Rose Masesa amesema Kaka yake alikuwa akiugua kwa muda mrefu, lakini hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri hadi juzi, kiasi kwamba familia ilitarajia angesafiri kwenda Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Masesa, hali ya Allute ilibadilika ghafla na kukimbizwa hospitalini ambako alifariki dunia “ndiyo mambo ya vifo, vinakupata wakati wowote, alizidiwa ghafla, akakimbizwa hospitali, alikuwa anaumwa muda mrefu, lakini hii ya kuzidiwa imetushtua sana na alikuwa anaendelea vizuri na tulijua anakuja Dar, tunamshukuru Mungu,” amesema Dada wa Marehemu.
Aidha, ameeleza kuwa Wakili Allute amefariki dunia katika Hospitali ya Siriani, Jijini Arusha na kwamba msiba kwa sasa upo nyumbani kwa Marehemu jijini humo, huku akibainisha kuwa hadi sasa hakuna ratiba rasmi ya mazishi iliyotolewa.
