
Makosa ya Kibinadamu Chanzo Cha AJALI ya Meli MV Mwanza
Serikali imebainisha kuwa makosa ya kibinadamu yalichangia ajali ya meli ya MV NEW MWANZA iliyotokea Novemba 18 baada ya kugonga miamba katika Ziwa Victoria.
Akitangaza matokeo ya uchunguzi wa Serikali, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameeleza kuwa uzembe na upungufu wa umahiri wa Nahodha katika mifumo ya uendeshaji vimechangia tukio hilo, huku akitoa maagizo mazito kwa Kampuni inayoendesha Meli hiyo.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo ya Novemba 18, Waziri Mbarawa amefafanua kuwa licha ya kugonga miamba, Meli ya MV NEW MWANZA haikupata madhara makubwa yanayoathiri uimara wake, udhibiti, wala mifumo yake ya uendeshaji.
Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mbarawa ameielekeza kampuni ya Meli (TASHICO) kumsimamisha kazi mara moja Nahodha aliyekuwa akiendesha Meli hiyo siku ya tukio. Vilevile, ameagiza kampuni ya Tashiko kufanya matengenezo ya meli hiyo chini ya uangalizi wa karibu wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) ili kuhakikisha usalama kabla ya kurejea kazini.
