Jeshi la Polisi Mkoani Tabora Lamkana Mkuu wa Kituo Cha Polisi Aliyemuomba Msamaha John Heche
Jeshi la Polisi mkoani Tabora limekanusha vikali kusambaa kwa video inayodai kuonesha “Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabora akiomba msamaha kwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA bara, John Heche baada ya vurugu,” likieleza kuwa taarifa hiyo ni ya uongo, yenye lengo la kupotosha umma na kudhalilisha mamlaka za usalama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, amesema Jeshi hilo halina afisa yeyote anayefanana na mtu aliyerekodiwa katika video hiyo ambayo imesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii wiki hii.
Kamanda Abwao amefafanua kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtu aliyerekodi video hiyo akijifanya ni Mkuu wa Kituo cha Polisi. Mtu huyo ni Daud Paul Delim (49), mkazi wa Mbagala A, Wilaya ya Igunga.
Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote kwa mujibu wa sheria za nchi, hasa zile zinazohusu uzushi, kughushi na uchochezi wa uongo kupitia mitandao.
Kamanda Abwao pia amewaonya wananchi dhidi ya kuamini kila wanachokiona au kusikia mitandaoni bila uthibitisho rasmi kutoka mamlaka husika, akieleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia teknolojia kueneza uzushi kwa lengo la kuchafua taswira ya vyombo vya dola.

