Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani kwa hasira na huzuni kubwa kitendo cha kinyama na kisicho cha kibinadamu kilichotekelezwa na Askari wa magereza, ambaye amemshambulia kwa kumsukuma kwa nguvu na kumuangusha Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Tundu Lissu, wakati akitoka katika viunga vya Mahakama ya Kisutu.
Taarifa iliyotolewa leo July 31,2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi CHADEMA, Brenda Rupia, imesema
“Tukio hili limetokea baada ya kuahirishwa kwa kesi ya uhaini kwa mara nyingine tena, ambayo sasa imepangwa kutajwa tena August 13, 2025, hili sio tukio la kawaida, ni tukio la kikatili, la kushtua, na linalodhalilisha utu wa binadamu”
“Ni hatari zaidi kwa kuwa limefanywa na Mtu ambaye, kisheria, anapaswa kuwa Mlinzi wa sheria, haki, ulinzi, na usalama wa raia wakiwemo wale wanaokabiliwa na kesi Mahakamani ambao bado wanastahili kuonekana kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo na vyombo vya sheria, ni muhimu kuwakumbusha Watanzania wote kwamba Mwenyekiti, Mh. Tundu Lissu, bado anaendelea kuishi na ulemavu wa kudumu uliotokana na kupigwa risasi 16 katika jaribio la mauaji la September 7, 2017”
“Kwa msingi huo, aina yoyote ya ukatili dhidi yake si tu kwamba ni kinyume cha sheria, bali pia ni tishio la moja kwa moja kwa maisha yake, CHADEMA inatoa wito mzito kwa Mahakama ya Tanzania, kama mhimili huru wa utoaji wa haki, kuhakikisha kuwa tukio hili linachunguzwa kwa kina, na hatua za haraka na wazi zinachukuliwa dhidi ya waliohusika, bila kujali wadhifa wao. Tukio la ukatili ndani ya maeneo ya Mahakama linaathiri taswira ya Mahakama kama kimbilio la haki, na linatishia uaminifu wa wananchi kwa mfumo wa utoaji haki nchini”

