Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, amewataka makada waliokatwa katika mchujo uliofanywa na Kamati Kuu ya CCM Taifa kuendelea kuwa wanachama watiifu na raia wema wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Julai 31,2025 jijini Dodoma kuhusu Mkutano Mkuu Maalum wa uchaguzi wa wabunge wa Viti Maalum na wawakilishi unaotajarijiwa kufanyika kesho kupitia Jumuiya hiyo, Hapi amesema ni muhimu kwa wanachama wote kuendelea kuwa wavumilivu na waaminifu kwa chama, hata pale ambapo hawakufanikiwa kuteuliwa.
“Niwaombe wanachama wote ambao hawajateuliwa kwenye mchujo uliofanywa na vikao vya juu vya maamuzi vya chama chetu, waendelee kuwa wavumilivu, watiifu na raia wema, wasiingie kwenye vishawishi vya kufanya maamuzi yasiyofaa,” amesema .
Akizungumzia Mkutano Mkuu Maalum wa Jumuiya hiyo, Hapi amesema maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa na jumla ya makada 33 wanatarajiwa kupigiwa kura na Wajumbe 756 ili kupata wabunge wa Viti Maalum.
“Walioteuliwa na chama ni 33, hii ni idadi kubwa sana, tunakishukuru chama chetu kwa mabadiliko ya Katiba yaliyowezesha majina 19 kurudi kugombea upande wa Bara, manane kwa Baraza la Wawakilishi, na sita kwa upande wa Zanzibar,” ameeleza Hapi.
Aidha, amewataka wagombea wote na wapambe wao kuzingatia maadili na kanuni za uchaguzi.
“Kwa atakayekiuka taratibu, chama na vyombo vya dola vitachukua hatua kali ili kuhakikisha tunapata viongozi bora na wenye sifa,” amesema Hapi.

