Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa agizo kwa makatibu wa mikoa wote nchini kuhakikisha wagombea wote wa nafasi za udiwani waliokuwa kwenye orodha ya awali wanarejeshwa kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Taarifa hiyo imetolewa siku ya Ijumaa na CPA Amos Gabriel Makalla, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, kufuatia kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Julai 31, 2025.
Katika kikao hicho, Sekretarieti ilijadili kwa kina malalamiko yaliyowasilishwa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu uteuzi wa wagombea wa udiwani, na hatimaye kuamua kufuta maelekezo yote ya awali yaliyohusu mchakato huo.
“Wagombea wote wa udiwani wa kata, waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni…wagombea wote waliopo kwenye orodha ya awali waliyotumiwa Makatibu wa Mikoa wa CCM, warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni”, imesema taarifa hiyo.
Aidha, CCM imewataka makatibu wa mikoa kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo mapya unafanyika kwa wakati, ili kuhakikisha mchakato wa kuwapata wagombea unakwenda kwa haki, uwazi na kwa mujibu wa taratibu za chama

