Nature

Cyprian Musiba Amkana Pole Pole Alia na Wabunge Mzigo

Mwanaharakati huru na mtia nia wa ubunge katika Jimbo la Mwibara mkoani Mara, Cyprian Musiba, amejitokeza kufafanua msimamo wake juu ya kile alichokiita ‘jaribio la makusudi la baadhi ya watu kumpachika uhusiano wa karibu na mwanasiasa Humphrey Polepole’, akisisitiza kuwa hana uhusiano wala mawasiliano naye kwa miaka mingi.

Akizungumza na Jambo TV, Musiba amesema kuwa kauli alizotoa hivi karibuni hazihusiani kwa namna yoyote na msimamo wa Polepole, ambaye amekuwa akieleza hadharani kukerwa na mwenendo wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akimtuhumu Rais Samia Suluhu Hassan na uongozi wa juu wa chama hicho kwa kile alichokiita ‘ukiukwaji wa haki, miiko na maadili ya chama’.

“Ninaomba ‘machawa’ wa CCM waache kuniunganisha na Polepole maana sina ukaribu naye wowote, na sina mazoea naye yoyote. Mimi niliongea kwa maslahi yangu mwenyewe na familia yangu na Watanzania kwa ujumla wanaoteseka kutokana na wabunge ‘feki’ wasiowajibika kwa wananchi wanaowachagua”, amesema Musiba kwa msisitizo.

Musiba ameeleza kuwa maumivu ya wananchi vijijini- ukosefu wa maji safi, umeme, na huduma za msingi licha ya rasilimali nyingi zilizopo ndicho kilichomsukuma kuwania ubunge. Hata hivyo, jina lake halikupitishwa na Kamati Kuu ya CCM, jambo ambalo amesema halitakata tamaa yake ya kuendelea kupigania haki na maendeleo ya wananchi.

Musiba amesema kuwa tofauti yake kubwa na Polepole ni kwamba yeye “hamshambulii Rais Samia,” bali huzungumza kwa staha na misingi ya maadili ya CCM.

“Tofauti yangu mimi na Polepole ni kwamba yeye anamshambulia Mhe. Rais wetu moja kwa moja, sasa sijui ni miiko gani na utamaduni gani huo kumshambulia Rais na Mwenyekiti wa chama ambaye amepitishwa na Mkutano Mkuu wa chama…ninachojua mimi utamaduni wa CCM Na: 1 ni kumheshimu Rais wa nchi na Mwenyekiti wa chama, sasa Polepole anamshambulia Rais, ninavyojua huo siyo utamaduni wa CCM tangu enzi na enzi”, amesema Musiba.

Ameongeza kuwa CCM imejengwa katika misingi ya kuvumiliana, kuheshimiana na kusikiliza sauti ya wananchi. Hivyo basi, mtu yeyote anayejaribu kutumia majina ya wengine kuhalalisha malalamiko binafsi “anafanya fitna kwa makusudi.”

Related Posts