
Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema kwa sasa siasa zimekuwa kama biashara kwani lazima uwe na mtaji wa kutosha ili kugombea nafasi yoyote, tofauti na kipindi alichoanza siasa.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha TBC leo Agosti 30, 2025, Sumaye amesema ili mtu agombee ubunge kwa sasa anapaswa kuwa na kiasi kisichopungua Shilingi milioni 300 hadi 500, na kwamba endapo hana kiwango hicho, hana nafasi ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha siasa.
“Leo unaambiwa kama huna milioni mia tatu, mia tano wala usijaribu, siasa imekuwa biashara, sisi zamani siasa haikuwa biashara,” amesema Sumaye.
Ameeleza kuwa tofauti na sasa ambapo wananchi huuliza mgombea atawaachia nini, enzi zake wananchi walijitolea kumsaidia mgombea, akisema walikuwa hadi wanachinja mbuzi kuwakaribisha wagombea kwenye mikutano ya kampeni.
Sumaye, ambaye alihudumu kama Mbunge wa Jimbo la Hanang kuanzia mwaka 1983 hadi 2005, amesema mara ya kwanza alipoamua kugombea ubunge alilazimika kukopa mshahara wa miezi miwili, jumla ya Shilingi 10,010 kutoka kampuni aliyokuwa akifanyia kazi.

