
Jeshi la Polisi nchini limekanusha vikali uvumi uliosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kupatikana kwa kontena lililosheheni silaha katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 1, 2025 Jijini Dodoma Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCP) David Misime, amesema kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na zina lengo la kupotosha umma pamoja na kuleta taharuki isiyo ya lazima.
Aidha katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, na kwamba mipaka yote ya nchi inalindwa kikamilifu huku akiwaomba wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa njia sahihi, kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa, na kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.
Taarifa hizo ambazo zimekanushwa na Jeshi la Polisi zilianza kusambaa baada ya mtumiaji maarufu wa mitandao ya kijamii Mange Kimambi kudai kupitia kurasa zake kwamba silaha za kivita na magari ya kifahari yameingizwa nchini kwa siri. Uvumi huo uliibua mijadala mikubwa na sintofahamu miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

