
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema amesema maisha yake yapo hatarini kwa sasa kwasababu kuna Watu wanamfuatilia hata kuonekana nyumbani kwake kitu ambacho kimemfanya awe na hofu na maisha yake.
Lema ameandika yafuatayo katika ukurasa wake wa X “Mheshimiwa Rais, maisha yangu yako katika hatari kubwa, tafadhali naomba kwa unyenyekevu mkubwa unisikilize, ningependa kuishi ili niweze kuwaona Watoto wangu wakikua, kuoa na kuolewa mbele ya macho yangu, na ikiwezekana, niweze kufurahia Wajukuu wangu ikiwa Mungu atanijalia maisha marefu, kila Mtu anatamani kuishi maisha marefu yenye amani na uzee mwema”
“Kwa sasa kuna Watu ambao wananifuatilia kwa karibu sana hata jioni ya leo wameonekana maeneo nyumbani kwangu na nina hofu kwamba wangeweza hata kumdhuru Mtu yeyote ambaye si mimi, kwa hali hii naona ni bora nijiweke mikononi mwa Mamlaka kwa hiari yangu kuliko kuendelea kuishi kwa hofu kila siku, niko tayari kuwekwa mahabusu kwa hiari yangu hadi kipindi cha uchaguzi kipite, kwasababu naamini kufanya hivyo kutaleta utulivu kwa Wazazi wangu, Mke wangu Neema na Watoto wangu, najua watahisi angalau faraja kwamba niko salama, ninaomba kwa moyo mkunjufu ulinzi na msaada wako, Mheshimiwa Rais”
Mwandishi wa @AyoTV_, Bakari Chijumba alipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ili kufahamu kama Lema ameripoti kuhusu kufuatiliwa na Watu hao ameeleza yafuatayo “Bahati mbaya sana siingii huko kwenye hizo (mitandaoni) kwahiyo sijaona hicho kitu, kwahiyo siwezi nikasemea chochote maana yake sijaona, maana yake sijui, maana yake sijaona hicho kitu unachosema”

