Katika kile kinachoonekana kuwa mabadiliko makubwa ya kiuongozi ndani ya serikali ya awamu ya sita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kumtangaza mrithi wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki hii. Majaliwa ameagizwa kutogombea tena ubunge, hatua inayoashiria mwisho wa safari yake kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.
Kwa mujibu wa Katiba, Rais atapendekeza jina moja la mgombea wa Uwaziri Mkuu na kulituma Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura ya uthibitisho. Kwa kuwa Bunge linadhibitiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), mchakato huo mara nyingi huwa wa kiitifaki zaidi kuliko ushindani wa kweli.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuwania nafasi hiyo ni Doto Biteko (46), Naibu Waziri Mkuu anayemaliza muda wake. Akiwa kijana mwenye ushawishi kutoka Kanda ya Ziwa, anatajwa kama chaguo dhahiri, japokuwa anakumbana na upinzani wa ndani ya chama na serikali.
Pia kuna Adolf Mkenda (63), waziri aliyewahi kushika wizara ya elimu na kilimo. Mkenda ni msomi wa uchumi na mtumishi wa muda mrefu wa serikali, anayesifika kwa uadilifu na misimamo ya kisheria. Anatoka Kanda ya Kaskazini.
Kitila Mkumbo (54), Waziri wa Uwekezaji na Mipango anayeondoka, pia ametajwa. Akiwa mwanasiasa aliyewahi kuwa wa upinzani na mhadhiri wa chuo kikuu, Kitila ni maarufu kwa kujenga hoja zenye mvuto kwa pande zote za kisiasa. Anatoka Kanda ya Kati.
Palamagamba Kabudi (69), msomi wa sheria na waziri wa zamani wa mambo ya nje na sheria, anatajwa kwa uzoefu na uaminifu wake kwa mamlaka. Kabudi pia aliongoza mazungumzo makubwa ya kiserikali kuhusu mikataba ya madini na gesi.
Jina jingine la kushangaza ni la Masanja Kadogosa, aliyewahi kuongoza Shirika la Reli Tanzania. Licha ya kutokuwa na uzoefu wa baraza la mawaziri, mchango wake kwenye mradi wa SGR umeongeza heshima kwake.
Majina ya mawaziri wa zamani kama George Simbachawene, Mwigulu Nchemba, Jumaa Aweso, na Anthony Mavunde pia yameanza kuzungumzwa, sambamba na Paul Makonda, aliyekuwa RC wa Dar es Salaam na Arusha.
Watanzania sasa wanasubiri kwa hamu kuona ni nani atayepewa jukumu hilo nyeti la kuongoza shughuli za serikali bungeni, huku Rais Samia akitarajiwa kuendelea kuimarisha safu ya uongozi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
