Yanga Yampiga Stop Denis Nkane Kwenda JKT Tanzania, TRA Ruksa

DILI la Denis Nkane kwenda JKT Tanzania, limeingia ugumu baada ya Yanga kukikunjia kikosi hicho, huku ikimtaka winga huyo asake timu nyingine atakayokwenda kwa mkopo lakini sio huko.

Nkane ambaye alitua Yanga Januari 2022 akitokea Biashara United, amekuwa hana nafasi kubwa ya kucheza kikosini hapo na klabu hiyo ina mpango wa kumtoa kwa mkopo wakati wa usajili wa dirisha dogo litakalofunguliwa Januari Mosi 2026.

Kukosa namba kwa Nkane kikosini hapo, kunatokana na uwepo wa Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Offen Chikola, Celestine Ecua ambao wamekuwa wakianza na kubadilishana mara kadhaa wakicheza nafasi anayomudu nyota huyo.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, Yanga imeweka ngumu kumruhusu Nkane kwenda kuchezea JKT kwani Makamanda hao wa Jeshi la Kujenga Taifa waliwahi kuwagomea kuwapa mastaa wao wawili.

Chanzo kutoka Yanga kimesema: “Yanga iliwahi kumhitaji Yakoub Suleiman aliyekuwa kipa wa kikosi hicho lakini mwisho alikwenda Simba, hivyo na kwao imekuwa ngumu kumuachia hata kwa mkopo.”

Wakati Yanga ikiikazia JKT Tanzania, inatoa mwanya kwa TRA United kuinasa saini yake kwani mabosi wa klabu hiyo ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Tabora United walikuwa wa kwanza kumuhitaji Nkane.

“Kwa sasa TRA ina nafasi kubwa zaidi ya kumpata Nkane, kwani ndiyo timu pekee ambayo inamhitaji na ilionyesha uthubutu wa kupeleka maombi,” kilisema chanzo.

Related Posts