
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limekanusha madai ya mama mzazi wa mwanaharakati, Godlisten Malisa kuwekwa chini ya ulinzi.
Polisi wamesema askari walifika nyumbani kwake kwa ajili ya uchunguzi wa taarifa iliyodai kuwepo kwa watu wenye silaha waliovamia makazi hayo usiku wa manane, katika Kijiji cha Old Moshi Kidia.
Kamanda Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema uchunguzi uliofanywa umehusisha maelezo ya viongozi wa Serikali ya Kijiji na Kitongoji, ambapo viongozi hao wamesema hawakuona wala kushuhudia magari yanayodaiwa kuhusika na tukio hilo huku wakielezwa kuwa walielezwa na mama huyo kuwa Novemba 22, 2025 aliona magari yakipita barabarani na kuyatilia shaka, hali iliyomsukuma kutoa taarifa Polisi.
Ameongeza kuwa uchunguzi umeonesha kuwa nyumba ya mama huyo iko karibu na barabara kuu ya Old Moshi Kidia, ambayo inatumika muda wote, hali inayosababisha magari mengi kupita eneo hilo na kwamba watu waliotoa maelezo hawakuthibitisha kuwaona watu waliofunika nyuso zao wala wenye silaha kama ilivyodaiwa.
