Mahakama Yaamuru Aliyegongwa na Mwendokasi alipwe mil 88/-

Mahamana Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeamuru Kampuni ya UDA Rapid Transport Ltd kumlipa fidia ya Sh. milioni 88.8 mwanamuziki na mpishi, Frank Zebaza, baada ya kugongwa na basi la mwendokasi na kupata majeraha makubwa yaliyomsababishia maumivu, mateso na kupungua kwa uwezo wa kujipatia kipato.

Mbali na hilo, mahakama imemwamuru dereva wa basi hilo, Hafidhi Ally, aliyebainika kuwa alikuwa akiendesha kwa mwendo hatarishi, kumlipa mlalamikaji Sh. milioni 10 kama fidia ya adhabu kutokana na uzembe wake uliosababisha ajali hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa Desemba 19, 2025 na Jaji Griffin Mwakapeje, kufuatia kesi ya madai namba 28992 ya mwaka 2024 iliyofunguliwa na Zebaza dhidi ya UDA Rapid Transport Ltd, dereva Hafidhi Ally, Shirika la Taifa la Bima (NIC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akidai fidia ya jumla ya Sh. milioni 600 kwa madhara aliyopata.

Katika madai yake, Zebaza aliomba alipwe Sh. milioni 350 kama fidia maalumu kwa gharama za matibabu na matumizi mengine yanayohusiana na ajali hiyo, Sh. milioni 150 kama fidia ya jumla kwa maumivu na mateso pamoja na Sh. milioni 100 kama fidia ya adhabu.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mwakapeje alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani unaonesha wazi kuwa mlalamikaji alipata majeraha makubwa yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji mkubwa na hadi sasa anaendelea kukumbwa na athari za kudumu katika mfumo wa fahamu na hisia, hali iliyosababisha kupungua kwa uwezo wake wa kufanya kazi.

“Majeraha haya yalimlazimu mlalamikaji kuhama kutoka Mbezi Makondeko kwenda Mikocheni kwa sababu za usalama na uangalizi wa kiafya.

“Aidha, ameshindwa kuendelea na shughuli zake za awali kama mwanamuziki na mpishi, hivyo kupoteza uwezo wake wa kujipatia kipato,” alisema Jaji Mwakapeje.

Mahakama ilibainisha kuwa ushahidi uliopo unaonesha mlalamikaji amepata hasara kubwa ya kiuchumi, kuporomoka kwa ubora wa maisha na kuendelea kuishi na maumivu na mateso ya muda mrefu, mambo yanayostahili kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

Kwa kuzingatia uzito wa majeraha na athari zake za kudumu, mahakama iliamua kuamuru mdaiwa wa kwanza, UDA Rapid Transport Ltd, kumlipa mlalamikaji fidia ya jumla ya Sh. milioni 85.

Vilevile, Jaji Mwakapeje alisema mahakama imeridhika kuwa mwendo hatarishi na uzembe wa dereva Hafidhi Ally, ambao ulithibitishwa kisheria baada ya kutiwa hatiani katika shauri la barabarani, unastahili kuadhibiwa kwa fidia ya adhabu.

“Mahakama inaona kuwa fidia ya adhabu ibebwe binafsi na mdaiwa wa pili. Hivyo, Sh. milioni 10 zitalipwa na dereva kama fidia ya adhabu,” alisisitiza jaji huyo.

Mbali na fidia hiyo, mahakama pia iliamuru UDA kumlipa mlalamikaji Sh. 3,850,600 kama fidia maalumu, pamoja na riba ya asilimia saba kwa mwaka kwa vipengele vya fidia ya jumla na fidia ya adhabu kuanzia tarehe ya hukumu hadi malipo yatakapokamilika.

Vilevile, gharama zote za kesi zimeamuriwa kulipwa kwa pamoja na UDA Rapid Transport Ltd na dereva Hafidhi Ally.

Katika mwenendo wa shauri hilo, ilielezwa kuwa baada ya kupokea hati ya madai, mdaiwa wa kwanza, wa tatu na wa nne waliwasilisha hati ya utetezi kwa pamoja wakikana kuwajibika na kuomba kesi itupiliwe mbali kwa gharama. 

Hata hivyo, mdaiwa wa pili hakuwasilisha utetezi wala kuhudhuria mahakamani licha ya juhudi mbalimbali kufanywa, hali iliyosababisha shauri kuendelea kusikilizwa pasi na kuwapo kwake.

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa, ajali hiyo ilitokea Septemba 30, 2022, wakati mlalamikaji alipokuwa akitembea kando ya Barabara ya Morogoro, eneo la Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo aligongwa na basi la mwendokasi aina ya Golden Dragon lenye namba ya usajili T132 DGW, linalomilikiwa na UDA.

Basi hilo lilikuwa limekatwa bima na Shirika la Taifa la Bima (NIC) na lilikuwa linaendeshwa na Hafidhi Ally kwa uzembe mkubwa, ikiwamo kuendesha kwa kasi kupita kiasi, kushindwa kuzingatia sheria za barabarani na kukosa udhibiti sahihi wa chombo hicho.

Kutokana na ajali hiyo, Zebaza alidai alipata majeraha makubwa ya kichwa yaliyosababisha jeraha dogo la ubongo (mild traumatic brain injury), kupoteza hisia ya kunusa, kuumwa kichwa mara kwa mara, kuathiriwa na mwanga mkali pamoja na kupungua kwa kumbukumbu.

Alieleza pia kuwa ameendelea kupata matibabu ya gharama kubwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), huku akipoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kuendelea na taaluma yake ya muziki na upishi.

Related Posts