Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uchaguzi Yaonya Wanaokwamisha Upatikanaji Ushahidi

Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 imewataka wananchi kupuuza vishawishi vyovyote vinavyolenga kuwazuia kutoa ushirikiano wao, ikieleza kuwa jitihada zozote za kuzuia utoaji wa maoni, ushahidi au taarifa zinahujumu juhudi za kitaifa za kutafuta ukweli na haki.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Desemba 26, 2025, Tume imeeleza kuwa imebaini kuwepo kwa watu au makundi ya watu yanayoshawishi wananchi kutojihusisha na kazi za Tume kwa kutoa maoni, ushahidi au taarifa muhimu. Tume imesisitiza kuwa ushawishi huo hausaidii mchakato wa kitaifa wa kuchambua yaliyotokea, kujifunza kutokana na makosa ya nyuma na kuweka msingi wa suluhu ya kudumu kwa Taifa.

Tume ambayo ipo chini ya Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Chande Othman imewahimiza wananchi kupuuza aina zote za vishawishi vinavyolenga kuwazuia kushiriki, na badala yake kutoa maoni, ushauri na taarifa kwa uwazi na hiari. Imeelezwa kuwa kupitia sauti za wananchi, Taifa linaweza kutambua changamoto zilizojitokeza, kuzitatua kwa misingi ya haki na kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii tena siku zijazo.

“Tume ya Uchunguzi ipo kwa ajili ya Watanzania wote, na mafanikio ya kazi yake yanategemea ushiriki mpana, wa hiari na wenye uwazi kwa wananchi. Amani, mshikamano na mustakabali salama wa Taifa letu ni jukumu la kila mmoja wetu”, imeeleza taarifa hiyo.

Related Posts