
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linafanya uchunguzi wa ajali ya magari mawili kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu watatu pamoja na majeruhi watano.
Ajali hiyo ilitokea Aprili 21, 2026 majira ya asubuhi katika eneo la Kona S, kitongoji cha Kikoni, kijiji cha Lumango, kata ya Kidodi, tarafa ya Mikumi, wilaya ya Kipolisi Ruhemba mkoani Morogoro, katika barabara kuu ya Mikumi–Kilombero.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, ajali hiyo ilihusisha gari aina ya lori (FAW) lenye namba za usajili T154 ECP/T229 EBY, lililokuwa likiendeshwa na Yasin Omary Nasiri (48), mkazi wa Dar es Salaam, likitokea Mikumi kuelekea Ruaha. Lori hilo lilipita bila tahadhari pikipiki ya magurudumu matatu (Toyo) iliyokuwa mbele yake katika mwelekeo huo huo, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na basi aina ya Tata lenye namba za usajili T996 EPP, mali ya kampuni ya ZL Supper, lililokuwa likiendeshwa na Emanuel Benito kutoka Ifakara kuelekea Dodoma.
Kutokana na ajali hiyo, watu watatu walipoteza maisha, akiwemo dereva wa lori hilo, Yasin Omary Nasiri (48), mkazi wa Dar es Salaam; Awadhi Ng’wana (60), fundi bomba, mkazi wa Mang’ula; pamoja na Zalaph Awadhi Ng’wana (20), mkazi wa Mang’ula.
Aidha, watu watano walijeruhiwa katika ajali hiyo. Majeruhi hao ni pamoja na mwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina lake anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 40 hadi 45; Amani Iddi (60), mkulima, mkazi wa Ifakara; Matha John (39), mfanyabiashara, mkazi wa Dodoma; Pendo Kui (68), mkulima, mkazi wa Singida; na Monica Lameck Mazuwameli (16), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lwemba, mkazi wa Lumango.
Majeruhi wote wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya St. Kizito iliyopo Mikumi.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyefanya kitendo cha kupita gari (overtaking) bila kuchukua tahadhari.
Jeshi la Polisi linaendelea kuwakumbusha madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepusha ajali na madhara yake. Aidha, limeonya kuwa hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya madereva wote wazembe.
