
Mtoto Nicolaus Mashaka (9), mkazi wa Mtaa wa Shunu, Kata ya Nyahanga katika Manispaa ya Kahama, amerejesha tabasamu baada ya kupatiwa matibabu maalumu na sasa kuanza kutembea, kufuatia takribani miaka miwili ya kulala kitandani kutokana na kuvunjika mguu wa kulia na kuharibika kwa mifupa.
Mashaka alipata nafuu hiyo baada ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye alisisitiza apelekwe katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa matibabu ya kibingwa, baada ya taarifa za kadhia yake kuripotiwa kwenye vyombo vya habari.
Awali, Nicolaus ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Nyahanga “B”, aliumia mguu alipokuwa akicheza mpira na wenzake. Badala ya kupelekwa hospitalini mara moja, alipelekwa kwa mganga wa jadi, hali iliyochelewesha matibabu na kusababisha mfupa kuharibika zaidi.
Baadaye alifikishwa Hospitali ya Manispaa ya Kahama na kisha kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando jijini Mwanza ambako alifungiwa vyuma mguuni. Hata hivyo, alihitaji matibabu ya kibingwa zaidi katika Taasisi ya MOI, jambo lililomfanya mama yake kuendelea kuomba msaada hadi Rais kutoa agizo la apatiwe matibabu stahiki.
Akizungumza Februari 4, 2026 katika ukumbi wa Manispaa ya Kahama, Ofisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Theresia Tarimo, amesema taasisi hiyo ilimpokea mtoto huyo Januari 5, 2026 akiwa hawezi kutembea na kuanza matibabu mara moja. Matibabu yalikamilika Januari 17 na mtoto akaanza mazoezi ya viungo.
“Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa agizo lake. Mtoto amepona na ameruhusiwa kurejea nyumbani, ingawa bado yupo chini ya uangalizi. Atatakiwa kurejea kliniki baada ya miezi mitatu na kwa sasa anaendelea kutumia dawa alizopewa,” amesema Tarimo.
Ameongeza kuwa mtoto huyo alifanyiwa upasuaji wa mfupa kwa nje na anaendelea vizuri, huku akisisitiza apunguze michezo na kuepuka kuumiza tena mguu wake.
Naye Ofisa Muuguzi wa Wodi ya Watoto MOI, Ritha Makundi, amesema Nicolaus alifanyiwa upasuaji mara mbili na kuwekewa kifaa saidizi kilichomwezesha kurejea katika uwezo wa kutembea.
Makundi pia amesema mama mzazi amepewa elimu ya afya ili kutambua dalili hatarishi, na kuwataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto hospitalini wanapoumia badala ya kukimbilia waganga wa jadi, jambo linaloweza kuchelewesha matibabu na kuongeza madhara.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Lusia Cosmasi, amesema hakuwahi kutarajia kumuona mwanawe akitembea tena, akieleza kuwa mfupa wa mguu wa kulia ulikuwa umeharibika vibaya hadi kulazimika kulala kitandani kwa miaka miwili.
Amesema sasa ataendelea na shughuli zake za kujipatia kipato ambazo zilikwama kutokana na kuhangaika kutafuta matibabu, na kuwasihi wazazi wengine kuwapeleka watoto hospitalini mapema wanapoumia ili kuepuka madhara makubwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Abrahaman Nuru, amesema halmashauri itamfuatilia mtoto huyo kwa karibu ili kuhakikisha anatumia dawa kwa wakati na kurejea kliniki kwa uangalizi kama ilivyoelekezwa.
Ameongeza kuwa mama huyo atapatiwa mkopo usio na riba kupitia programu za ndani za halmashauri ili kumwezesha kurejesha shughuli zake za kiuchumi.
Kuhusu masomo, Nuru amependekeza mtoto aanze shule baada ya sikukuu za Pasaka ili kufuatilia kwanza mwenendo wake wa kiafya, hoja iliyoungwa mkono na wataalamu wa afya wa MOI.
