
Wakala mmoja wa Benki aitwae Paulo Akweso Mkazi wa Songea Mkoani Ruvuma, amekimbilia mikononi mwa Polisi kuomba msaada baada ya kutapeliwa kiasi cha Tsh. milioni 147.3 na Watu watatu waliojifanya Viongozi wa dini waliomuaminisha kuwa pesa hizo zitaongezeka baada ya kuchukuliwa na Malaika.
Wakala huyo wa Benki alidanganywa na Matapeli hao kuwa achukue pesa hizo Tsh. milioni 147.3 cash azipeleke katika chumba maalumu cha Guest House kisha aziache hapo ambako Malaika watazichukua na kuzibariki kisha kuzirudisha zikiwa zimeongezeka mara mbili yake.
“Kwa kuamini Wakala huyo alipeleka pesa hizo na badaye akagundua zimeshachukuliwa na ameshatapeliwa” Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma limefanikiwa kuwakamata katika maeneo tofauti ya Uhindini Dodoma na Mbinga Mkoani Ruvuma Watuhumiwa hao wa utapeli.
Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma limetoa tahadhari juu ya utapeli huo wa kutumia dini na imani na kuwataja Watu hao watatu akiwemo Onesco Kelvin Kangapi maarufu Boss hanuniwi ambaye ni Kiongozi wa Matapeli hao ambaye akaunti yake ya Benki imekutwa na Tsh. milioni 88 ambazo ni miongoni mwa pesa walizotapeli kwa Kelvin na pesa nyingine amenunua pikipiki nne na viwanja vitatu huko Mbinga.
