Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimetoa tamko rasmi kuhusu matukio yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025, kikisisitiza umuhimu wa kuheshimu utawala wa sheria, wajibu wa raia, na mipaka ya matumizi ya haki za binadamu nchini.
Kupitia tamko lililotolewa leo Novemba 12, 2025, TPBA imesema kimechunguza kwa kina taarifa na tuhuma mbalimbali zilizotolewa na taasisi na mashirika ya haki za binadamu, kikieleza kuwa haki na uhuru wa mtu binafsi lazima vitumike bila kuathiri usalama wa taifa au kuvunja haki za wengine.
“Kama ilivyoelezwa na Ibara ya 30(1) ya Katiba, haki na uhuru wa binadamu havitumiwi kwa namna inayosababisha kuingiliwa kati kwa haki na uhuru wa watu wengine au kuvuruga maslahi ya umma,” kimesema chama hicho katika taarifa yake.
TPBA imefafanua kuwa maandamano yaliyofanyika Oktoba 29, 2025 hayakuwa halali kwa mujibu wa sheria, kwa kuwa yalikiuka zuio lililotolewa na Jeshi la Polisi kwa sababu za kiusalama, na kwamba ushahidi unaonesha baadhi ya maandamano hayo yaligeuka vurugu, yakiambatana na uharibifu wa mali, mashambulizi kwa askari, na uchomaji vituo vya kupigia kura.
Kuhusu tuhuma za matumizi ya nguvu kupita kiasi na vifo vilivyotokea, TPBA imesisitiza kuwa matumizi ya silaha au risasi ni hatua ya mwisho (last resort) inayoruhusiwa kisheria pale tu mbinu nyingine zote zikishindikana.
“Uwajibikaji wa vyombo vya dola ni sehemu ya utawala wa sheria, na uchunguzi wa haki unapaswa kufanyika pale panapotokea tuhuma za matumizi ya nguvu za ziada, kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais wakati wa hotuba yake ya uapisho Novemba 3, 2025,” taarifa hiyo imeongeza.
TPBA pia imezungumzia changamoto za upatikanaji wa huduma za intaneti wakati wa uchaguzi, ikieleza kuwa hatua ya kusitisha au kudhibiti mawasiliano kwa muda inaruhusiwa kisheria pale inapolenga kulinda usalama wa taifa au kuzuia uvunjifu wa amani.
Aidha, chama hicho kimeonya vyama vya siasa na taasisi zinazohusishwa na vurugu kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 20(2) ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa, chama chochote kinachoshiriki au kushinikiza uvunjifu wa amani kinaweza kufutiwa usajili na viongozi wake kuwajibishwa kisheria.

