Clemence Mwandambo Afikishwa Mahakamani, Aachiwa Kwa Dhamana

Mwanaharakati wa mitandao ya kijamii na mwalimu wa shule ya chekechea, Clemence Kenan Mwandambo, ambaye alikuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 29, 2025, ameachiwa kwa dhamana baada ya kufikishwa kwa siri katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam na kusomewa maombi ya kuwa chini ya uangalizi wa mahakama (Binding Over).

Kwa mujibu wa Wakili wake, Hekima Mwasipu akizungumza na Jambo TV, Mwandambo alifikishwa mahakamani hapo Januari 9, 2026 bila ndugu zake wala mawakili wake kufahamu, licha ya juhudi za muda mrefu za kuisaka taarifa ya mahali alipokuwa akishikiliwa tangu alipokamatwa mkoani Mbeya. Wakili Mwasipu amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya halikuwa wazi kuhusu eneo alikohifadhiwa Mwandambo, hali iliyowafanya kushindwa kupata taarifa sahihi kwa zaidi ya siku kumi.

Amesema katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi ya Binding Over ukiiomba mahakama itoe amri kadhaa, ikiwemo Mwandambo kutotenda kosa lolote kwa kipindi cha mwaka mmoja, kuripoti katika Kituo cha Polisi Mbeya kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari 9, 2026, pamoja na kutoa akaunti zake zote za mitandao ya kijamii kwa Jeshi la Polisi.

Baada ya kusikiliza maombi hayo, mahakama ilikubaliana na upande wa Jamhuri na kutoa amri hizo. Hata hivyo, kwa kuwa Mwandambo hakuwa na wakili wala ndugu mahakamani, na hakuna aliyekuwa akijua alikokuwa akishikiliwa, alirejeshwa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe baada ya kutoka mahakamani, kabla ya ndugu zake kupigiwa simu siku iliyofuata ambayo ni leo Jumamosi Januari 10, 2026 na kuombwa kumdhamini, hatua iliyosababisha kuachiwa kwake.

Wakili Mwasipu amesema Mwandambo kwa sasa yuko nje kwa dhamana na yupo chini ya uangalizi kwa mujibu wa amri za mahakama, huku akibainisha kuwa Jumatatu ijayo watafanya kikao na mteja wao ili kujadili hatua za kisheria zitakazofuata kwa lengo la kuhakikisha haki zake za msingi zinalindwa.
View all 75 comments

Related Posts