Gari iliyowagonga watu wawili.
Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia mmiliki wa daladala baada ya dereva aliyekuwa anaiendesha kukimbia baada ya kuwagonga watu wawili, akiwemo askari wa usalama barabarani.
Aliyekamatwa ni Mohamed Mumpa (40), mkazi wa Isamilo jijini Mwanza, ambaye ni mmiliki wa daladala aina ya Toyota Hiace, inayofanya safari zake kati ya Kakobe – Airport wilayani Ilemela.
Dereva huyo ambaye amefahamika kwa jina moja la Alphonce amekimbia baada ya kusababisha ajali hiyo iliyotokea saa 2:00 asubuhi katika eneo la mzunguko wa Mwanza Hotel, barabara ya Kenyatta jijini Mwanza.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema daladala hiyo iliyokuwa imebeba abiria, ikitoka Kakobe kuelekea Airport, iliacha njia na kuserereka kisha ikawagonga watu hao.
“Gari hilo liliacha njia na kuserereka upande wa kushoto wa barabara, likagonga gema kisha likamgonga askari wa Jeshi la Polisi ambaye alikuwa amesimama pembeni akifanya kazi yake ya usalama barabarani (kuongoza magari), pamoja na mtembea kwa miguu aliyekuwa anapita eneo hilo,” amesema Mutafungwa.
Mutafungwa amemtaja askari aliyegongwa kuwa ni mwenye namba F7768 Koplo Tumsifu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana, pamoja na Lucia Densiana (31), mkazi wa Mahina jijini Mwanza, ambaye ajali imemkuta alipokuwa akielekea kwenye shughuli zake za ujenzi wa taifa.
Amesema baada ya ajali hiyo dereva aliteremka na kukimbia huku akiwaacha abiria, kabla ya askari pamoja na wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo kuingilia kati.
Mutafungwa ameongeza kuwa majeruhi hao walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, ambako wanaendelea kupata matibabu.
“Uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na msako mkali unaendelea kufanyika kumtafuta dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo. Gari hilo pia linaendelea kufanyiwa uchunguzi na wakaguzi wa magari ili kubaini kama lilikuwa na hitilafu zozote, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa,” amesema.
Akieleza sababu za kumkamata mmiliki wa gari hilo, Mutafungwa amesema wamechukua hatua hiyo ili awasaidie kumtafuta dereva huyo kwa kuwa ndiye alimwajiri na ana kumbukumbu za taarifa zake.
“Tumemshikilia kwa lengo la kumhoji kwa sababu ana wajibu wa kutunza kumbukumbu za taarifa za dereva aliyemuajiri, ambaye hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta,” amesema Mutafungwa na kuongeza;
“Kwa hiyo tumemshikilia ili atusaidie kuhakikisha dereva anapatikana na hatua kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za usalama barabarani,” amesema.
Kamanda Mutafungwa amewataka madereva wanaoendesha magari jijini Mwanza kuendelea kuzingatia kanuni na taratibu za usalama barabarani, kuendesha kwa kufuata sheria na kuwajali watumiaji wengine wa barabara.
