Dawa Kulevya Zawekwa Kwenye Bidhaa Tamu Kuvutia Watoto

Dawa Kulevya Zawekwa Kwenye Bidhaa Tamu Kuvutia Watoto
Dawa Kulevya Zawekwa Kwenye Bidhaa Tamu Kuvutia Watoto

Raia wa kigeni waliokamatwa Zanzibar kwa tuhuma za kujihusisha na usambazaji dawa za kulevya.
MAMLAKA ya Udhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) imebaini mbinu mpya ya usambazaji wa dawa za kulevya kwa kuzichanganya katika bidhaa za kawaida za matumizi ya kila siku, na kuwakamata watu watatu akiwemo mwekezaji anayehusishwa na mtandao huo.

Amesema uchunguzi wa kitaalamu umebaini kuwa dawa hizo zimechanganywa kwenye bidhaa zenye vifungashio vya kuvutia na ladha mbalimbali kama grape ice, mango ice na strawberry ice, zikilenga kuwavutia watoto na vijana bila kufahamu hatari iliyomo ndani yake.

Hayo yamebainishwa leo Migombani, Mjini Zanzibar, na Kamishna wa ZDCEA, Kanal Nassor Burhan, akisema operesheni maalum ilifanyika Januari 25 na 29 mwaka huu katika maeneo ya Paje, Jambiani, Bweni na Shangani.

“Ukaguzi ulifanywa katika maduka ya Popeyes UK Treatz, Shop N’go na ghala la Mpendae baada ya kupatikana taarifa za kijasusi.

“Bidhaa hizo zilikuwa zikiuzwa kwa bei ya juu isiyo ya kawaida, hali inayoashiria uwepo wa dawa za kulevya ndani yake. Kwa mfano, pipi moja ilikuwa ikiuzwa 100,000 tofauti na bei ya kawaida ya pipi sokoni,” amesema.

Kamishna huyo amesema dawa hizo zinaingizwa nchini na raia wa Romania, Alexandru Rozescu, kupitia uwekezaji wake wa Zebra Retail Investment, na kusambazwa Zanzibar, Tanzania Bara na baadhi ya nchi jirani.

Amesema mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake akiwemo Nahid Bandar Imtiz (33) na Farhad Mustafa Gulam (33) tayari wamefikishwa mahakamani.

Pia kamishna ameonya kuwa iwapo hazitadhibitiwa, dawa hizo zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya na kijamii ikiwemo kuongezeka kwa waraibu wapya, matatizo ya afya ya akili, vifo vya ghafla na kuongezeka kwa uhalifu.

Aidha, amewataka wazazi na wananchi kuwa makini na bidhaa wanazowanunulia watoto na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapobaini viashiria vya bidhaa zenye shaka.

Related Posts