
Rais wa Marekani, Donald Trump ameiagiza Pentagon na Idara nyingine, kuanzisha mchakato wa kutambua na kuachilia nyaraka zote za Serikali zinazohusiana na Viumbe wa ajabu kutoka nje ya Dunia ( aliens ), agizo ambalo limekuja siku chache tangu Rais wa zamani Barack Obama kuulizwa na kusema “Wapo kweli lakini sijawaona”
Rais Trump ambaye akiwa kwenye mahojiano yaliyofanyika kwenye Ndege ya Air Force One alisema kitendo cha Barack Obama kuongelea taarifa za siri kwenye mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni ni makosa makubwa na kwamba hakutakiwa kufanya alichofanya, ambapo sasa amelazimika kutoa agizo hili kutokana na shauku kubwa ya Umma juu ya masuala hayo.
Rais Trump alipoulizwa kama anatambua uwepo wa viumbe hao alijibu “sijui kama wapo kweli au la” ambapo hadi sasa hakuna ushahidi au picha halisi za viumbe hao isipokuwa taswira iliyopo ni picha za kutengeza na zile ambazo hutumika kwenye filamu za hollywood ( kama hii inayoonekana mwanzoni mwa chapisho hili )
Katika miaka ya karibuni Marekani imeshuhudia ongezeko la hamu kubwa ya Raia wake wakitaka kufahamu ukweli Viumbe hao wa ajabu na maisha ya nje ya dunia ambapo shauku hiyo imechochewa na tukio la mwaka 2017 na ripoti kuhusu mpango wa siri wa Pentagon wa kuchunguza ushuhuda wa Marubani na Wanajeshi wengine wa Marekani walioripoti kuona vitu vya ajabu angani.
Mnamo mwaka 2022 Bunge la Marekani lilifanya mkutano wa kwanza baada ya kupita miaka 50 kuhusu UFOs (Vitu visivyo vya kawaida vinavyoruka ) huku Makao ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ikiahidi uwazi zaidi katika suala hilo na kuanzisha Ofisi maalumu ya kukusanya ripoti zote za mawasiliano ya kijeshi na UFOs ambapo mwaka uliofuata, Kamati ya Bunge la Marekani ilichunguza mada hiyo bila kupata matokeo makubwa au uthibitisho wa maisha ya kigeni ambapo katika ripoti ya 2024, Pentagon ilisema kuwa hakuna ushahidi kwamba serikali ya Marekani imekutana na Viumbe wa kigeni na kwamba matukio ya UFO yalikuwa ya vitu vya kawaida tu.
