
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza kusitisha kwa muda wa siku tano mipango yote ya kijeshi ya kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran, kufuatia kile alichokielezea kama mazungumzo “mazuri sana na yenye tija” yaliyofanyika ndani ya siku mbili zilizopita kati ya mataifa hayo mawili.
Kupitia ujumbe wake (kwa herufi kubwa) alioutoa leo, Trump amebainisha kuwa sauti ya mazungumzo hayo ya kina yanamfanya aamini kuwa kuna uwezekano wa kufikia suluhu ya kudumu ya uhasama uliopo Mashariki ya Kati.
Rais Trump ameiagiza wizara yake ya ulinzi kusitisha mashambulizi yaliyokuwa yamepangwa dhidi ya vinu vya umeme na miundombinu ya mafuta ya Iran, ili kutoa nafasi kwa timu za majadiliano kuendelea na kazi hiyo wiki nzima.
“Nimefurahi kuripoti kuwa Marekani na nchi ya Iran zimekuwa na mazungumzo yenye tija kuelekea suluhu ya jumla ya uhasama wetu. Kufuatia mazungumzo haya ya kina na ya kujenga, nimeelekeza kuahirisha mashambulizi yoyote ya kijeshi kwa kipindi cha siku tano,” ameandika Rais Trump.
Tangazo hili limekuja wakati saa 48 za sharti la awali la Trump zikikaribia kuyoyoma. Kusitishwa huku kwa mashambulizi kunatarajiwa kupunguza taharuki katika Mlango-Bahari wa Hormuz na kunaweza kusaidia kushusha bei ya mafuta ambayo ilikuwa imeanza kupaa kutokana na hofu ya vita vya jumla.
