Drogba Atoa Kauli Kupokonywa UBINGWA Senegal

Mshambuliaji wa zamani wa Timu Ya Taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, ameonyesha kusikitishwa na uamuzi wa CAF kuwavua ubingwa wa AFCON 2025 na kuwapa Morocco kitendo alichotaja kinaathiri uaminifu, utu na roho ya soka la Afrika Drogba katika taarifa aliyochapisha katika mitandao ya kijamii leo Jumatano Machi 18, 2026, ameeleza kuwa maamuzi yanapochukua muda mrefu baada ya filimbi ya mwisho huleta mashaka na maumivu makubwa. “Ndugu zangu, kuhusu soka la Afrika leo nazungumza kwa moyo mzito.

Mwezi Januari, sote tulitazama Senegal ikipambana kwa ujasiri na kuishinda Morocco katika fainali ya kihistoria. Ulikuwa usiku wenye shauku kubwa na fahari kwa bara zima. Kuanzia Dakar hadi Abidjan, kutoka Lagos hadi Nairobi, Afrika iliidhinisha mabingwa wake. Miezi kadhaa baadae, Bodi ya rufaa imebadilisha hadithi. Imebadilisha matokeo na ghafla ushindi uliopatikana uwanjani unaondolewa.

Hii inaathiri uaminifu, utu na roho ya soka la Afrika. Ndiyo, sheria lazima ziwepo, Nidhamu lazima iwepo lakini maamuzi yanapochukua muda mrefu baada ya filimbi ya mwisho huleta mashaka na maumivu makubwa. Wanafanya Dunia ihoji kuhusu Shirikisho letu na umoja wetu. Nyakati kama hizi, wakosoaji watazitumia ili kudharau Kombe la Mataifa la Afrika na kupunguza ukubwa na umuhimu wake. Afrika sio ndogo.

Afrika imetoa wachezaji wakubwa ambao wameshinda Ulaya na kuhamasisha mamilioni ya waafrika, Kutoka kwa Samuel Eto’o hadi kwa Mohamed Salah, kutoka Sadio Mane hadi kwa Riyad Mahrez. Vipaji vyetu havina mashaka. Tunachohitaji sasa ni uongozi unaolinda sura yetu nzuri ya mchezo wetu, Uongozi unaojenga uaminifu, uwazi na utulivu kwa kizazi kijacho.

Kama haki lazima itolewe basi iombwe hata mbele ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS). Lakini pia tuangalie ndani yetu na kuulizana. Je, tunajenga mustakabali gani kwa soka la Afrika? Mashabiki wanajitoa, Wachezaji wetu wanatoa kila kitu kwaajili ya nembo zao na Mataifa yao. Hatupaswi kuruhusu siasa kuiba furaha ya ushindi kutoka kwa watu wetu. Afrika inastahili heshima. Soka la Afrika linastahili misingi imara. Sisi ni watu wakubwa lazima tusimame pamoja”

Related Posts